NEWS

Monday 14 March 2022

LEAT kuwashtaki waliochafua mto Mara



CHAMA cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira Tanzania (LEAT) kimesema kinafuatilia kwa karibu tukio la uchafuzi wa mto Mara na kwamba liko tayari kuwashtaki watakabainika kuhusika na uchafuzi huo.

“LEAT iko tayari kushirikiana na wadau wengine katika kuchukua hatua za haraka za kuulinda Mto Mara.

“Hatua hizo ni pamoja na kufungua mashtaka mahakamani dhidi ya yoyote yule atakayebainika kuhusika na uchafuzi wa Mto Mara,” Afisa Miradi wa LEAT, Clay Mwaifwani ameiambia Mara Online News leo.

Mwaifwani amesema Sheria ya Tanzania ya Usimamizi wa Mazingira Na. 20 ya Mwaka 2004 inatoa nafasi kwa mtu yoyote kufungua shauri mahakamani iwapo mazingira yanachafuliwa.

“Suala la uchafuzi wa mazingira ni kosa kisheria, si kwa sababu lina athari hasi kwa mwanadamu pekee, bali kwa sababu linaathiri pia hadhi ya mfumo ikolojia,” amesisitiza.

Tukio la uchafuzi wa mto Mara unaotiririsha maji kwenye Ziwa Victoria, liliripotiwa hivi karibuni, sambamba na vifo vya samaki katika eneo la Kirumi darajani

Mamlaka zimezuia wananchi waishio jirani na eneo hilo kutumia maji na samaki, kufanya shuguli za uvuvi, unweshaji mifugo na kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia maji ya mto huo.

Wananchi hao wameanza kulalamika kukosa huduma ya maji kwa urahisi, baada ya kupigwa marufuku kutumia maji ya mto huo.

“Tumeambiwa tusitumie maji ya mto Mara lakini hakuna mbadala na tuna shida sana ya kupata huduma ya maji kwa sasa,” Mwenyekiti wa jumuiya ya watumia maji ukanda wa Mara Kaskazini, Siproza Charles ameiambia Mara Online News.

Watu wengi wameeleza kushtushwa na jinsi uchafuzi huo ulivyotokea.

“Tulishangaa maji yanageuka rangi kuwa meusi na samaki wanakufa kwa wingi, sasa hakuna samaki na tumezuiwa kuwatumia,” mkazi mwingine wa eneo hilo amelalamika.

Mmoja wa wanawake waishio jirani na mto huo, anayejishughulisha na biashara ya kuuza chakula amesema “Sasa hivi kitoweo ni nyama, samaki basi tena.”

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) Ijumaa iliyopita, tukio hilo lilisababishwa na mafuta na grisi.

“Kwani kuna utaratibu wa kumwaga, mafuta na grisi mto Mara inakuwaje, au kuna gari lilipata ajali mtoni?” mmoja wa wananchi amehoji baada ya kuona taarifa hiyo kwenye mitandao ya kijamii.

Taarifa hiyo ya LVBWB, ilisema uchunguzi wa kimaabara umebaini kuwa uchafuzi huo ulisababishwa na kiwango kikubwa cha mafuta na grisi kuliko kinachotakiwa kwa mujibu wa viwango vya ubora wa maji Tanzania.

Sababu nyingine kwa mujibu wa wa taarifa hiyo, ni kukosekana kwa hewa ya oksijeni kwenye maji kuliko kiwango kinachokubalika kwa mujibu wa viwango vya ubora wa maji Tanzania.

Taarifa hiyo imeibua mjadala mpana katika mitando ya kijamii, huku wananchi wakitaka mamlaka zenye dhamana ya maji na mazingira kuweka hadharani chanzo cha mafuta na grisi vilivyochafua mto huo ambao unategemewa na maelfu ya wananchi na wanyamapori katika ikolojia ya Serengeti.

“Kwa kuwa kamati imuendwa tusubiri majibu, lakini tunachojua hakuna viwanda jirani na mto Mara tofaufati na migodi. Waende migodini kuona kama kuna mabomba yanayotema maji machafu ndani ya mto Mara,” alisema ofisa wa serikali alipozungumza na Mara Online News, kwa sharti la kutotwajwa jina gazetini juzi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo alifika eneo la tukio Ijumaa iliyopita na kutangaza kuunda kamati ya kitaifa ya watu 11 na kupa siku saba kuchunguza chanzo cha uchafuzi wa maji na vifo vya samaki katika mto Mara.

Waziri Jafo ameitaka kamati hiyo kufanya kazi kwa uhuru na ipatiwe ushirikiano na wadau wote.

Mamlaka zimepiga marufuku wananchi kutumia maji ya mto huo kwa mahitaji yoyote baada ya uchafuzi huo kutokea.

Kutokana na hali hiyo, Waziri Jafo ameitaka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kutafuta mbadala wa upatikanaji wa maji kwa ajili ya wananchi wanaishio jirani na mto Mara wakati uchunguzi zaidi ukiendelea.

Mbunge Rorya aomba visima
Wakati huo huo, Mbunge wa Rorya, Jafari Chege ameiomba Wizara ya Maji kusaidia mamia ya wakazi wa vijiji vilivyoathirika kutokana na uchafuzi wa mto Mara, kupata huduma ya maji mbadala.

“Namuomba Waziri wa Maji [Jumaa Aweso] kutoa fedha kugharimia uboreshaji wa visima vilivyopo na kuchimba vingine katika vijiji vilivyoathirika,” Mbunge Chege amesema katika mazungumzo na Mara Online News kwa njia ya simu.

Mbunge wa Rorya, Jafari Chege

Mamla katika wilaya za Rorya na Butiama mkoani Mara zimezuia wakazi wa vijiji vilivyo jirani na maeneo yaliyokumbwa na uchafuzi kutumia maji na samaki katika mto Mara, kwa usalama wa afya na maisha yao.

Hatua hizo zilichukuliwa siku chache baada ya maji ya mto Mara eneo la Kirumi darajani kubadilika rangi kuwa meusi, huku samaki wakionekana kuelea wakiwa wamekufa, hali iliyozua taharuki kubwa kwa wananchi.

Mbunge Chege amesisitiza kuwa zuio hilo ni muhimu kwa usalama wa afya na maisha ya wananchi hao, hivyo kuomba huduma ya maji mbadala kwa ajili yao.

“Maji ni uhai, siku zinakwenda wananchi hawana maji,” amesema.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages