NEWS

Monday 14 March 2022

Mfuko wa Dhamana North Mara wawazawadia wanafunzi waliopata division 1 kidato cha 4MFUKO wa Dhamana North Mara umekabidhi zawadi za vyeti na fedha taslimu kwa wanafunzi 20 waliopata ufaulu wa daraja la kwanza katika mtihani wa taifa wa kuhitimu kidato cha nne mwaka 2021.

Wanafunzi hao wakiwemo wasichana watano, wamekabidhiwa zawadi hizo katani Nyamwaga jana, katika hafla iliyoandaliwa na Kikundi cha Vijana cha Wings (Wings Youth Group - WYG) Nyamongo.

Wanatoka katika shule za sekondari Nyamwaga Hill, Ingwe, Bwirege, Kibasuka, JK Nyerere, Nyamongo, Kemambo na Genge - zilizopo jirani na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.

Mgeni rasmi, Meneja wa Mfuko huo, John Waigama na wenzake, wamekabidhi fedha taslimu shilingi 200,000 kwa kila mwanafunzi kutokana na ufaulu wa daraja la kwanza (division one), huku baadhi yao pia wakizawadiwa shilingi 50,000 kwa kila alama A ya ufaulu.

Aidha, shule hizo zimezawadiwa shilingi 200,000 kwa kila daraja la kwanza, huku walimu ambao masomo yao yalipata ufaulu wa alama A wakizawadiwa shilingi 50,000 kwa kila A.

“Wazazi tutumie fursa zilizopo kusomesha watoto wetu, wafike mahali waweze kuibadilisha jamii yetu kimaendeleo,” Wegama amesema katika hotuba yake.
Waigama akihutubia katika hafla hiyo
Kwa upande wake, mlezi wa wa kikundi cha Wings Youth Group Nyamongo, Nicodemus Keraryo ameupongeza Mfuko huo na kikundi hicho kwa juhudi kubwa kutokana na kuhamasisha ukuaji wa elimu katika jamii inayozunguka mgodi wa North Mara.
Keraryo (aliyesimama) akizungumza katika hafla hiyo
Nao wazazi na walimu walioshiriki hafla hiyo, wamezipongeza taasisi hizo za kijamii kwa kuchochea ukuaji wa taaluma kwa wanafunzi, huku wakibainisha kuwa wengi wa wanafunzi waliofaulu na kupewa zawadi hizo ni ambao walikuwa wakitembea umbali mrefu kwenda shule na kurudi nyumbani.

Awali, Makamu Mwenyekiti wa Wings Youth Group Nyamongo, Yusuph Gesase amesema kikundi hicho kimejikita katika kuhamasisha maendeleo ya jamii, ukiwemo ukuaji wa taaluma katika shule hizo.

“Zawadi hizi ziwafanye wanafunzi hawa na wengine kusoma kwa bidii ili waweze kufanya vizuri zaidi katika mitihani ya kitaifa,” Gesase amesema.
Gesase akizungumza katika hafla hiyo
(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages