NEWS

Friday 18 March 2022

Mafunzo ya kuzuia rushwa: TAKUKURU Tarime yawapa vijana mwongozo, DC atia nenoTAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Tarime, Mara imetambulisha rasmi mwongozo wa mafunzo ya kupambana na rushwa kwa vijana wa skauti wilayani hapa.

“Tumeanza na viongozi wa skauti na wataalamu wa elimu, matarajio yetu ni kuifikisha elimu hii katika shule na ndani ya jamii ili kuongeza uelewa kwa wananchi waweze kutoa taarifa dhidi ya vitendo vya rushwa,” Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Tarime, Protas Sambagi amesema katika mkutano wa kutambulisha mwongozo huo mjini hapa, juzi.

Sambagi amesema vijana wa skauti watasaidia kueneza mafunzo hayo katika shule za msingi na sekondari.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele (pichani juu aliyesimama) amesema mafunzo hayo yatasaidia kuwafanya vijana kuchukia rushwa wakiwa wadogo na kuwa na uzalendo kwa taifa.

"Wahenga walisema samaki mkunje angali mbichi na mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, ndiyo maana zimeanzishwa klabu za wapinga rushwa katika shule za msingi, sekondari na vyuo ili kuwa na vijana na hatimaye taifa la watu waadilifu, wawajibikaji na wazalendo wanaochukia rushwa na maovu yote katika jamii,” amesema Mntenjele.

Ametumia fusa hiyo kuwataka maofisa elimu kutoa maelekezo kwa wakuu wa shule kuhusu umuhimu wa maudhui ya mwongozo huo ili uweze kuzaa matunda.

Kwa upande wake, Katibu wa Skauti Wilaya ya Tarime, Julius Ally amesema wamepokea mwongozo huo na kwamba watashirikiana na TAKUKURU kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa kupitia elimu.

Wilaya ya Tarime inakadriwa kuwa na vijana wa skauti 500 kwa sasa.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages