NEWS

Thursday 10 March 2022

Miradi inayotekelezwa chini ya RUWASA kunufaisha maelfu ya wananchi Serengeti


MAELFU ya wananchi wilayani Serengeti, Mara wanatarajiwa kunufaika na huduma ya maji safi na salama, kutokana na miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 6.2 inayotekelezwa na Serikali katika vijiji 20, chini ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

Kwa mujibu wa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Serengeti, Mhandisi Deus Mchele, miradi hiyo iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji na inatarajiwa kukamilika Juni mwaka huu.

Mhandisi Mchele

Mhandisi Mchele ametaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na uchimbaji wa kisima cha maji chenye urefu wa mita 150 na utandazaji mabomba kwa urefu wa kilomita tano kwenda kwenye tenki katika kijiji cha Kebanchabancha.

Fundi akifuatilia mtambo ukichimba kisima katika kijiji cha Kebanchabancha

“Kwa sasa wakazi wa kijiji cha Kebanchabancha wanalazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji kwenye mito, mabwawa na visima vya asili. Mradi huu wa RUWASA ukikamilika utanufaisha wananchi 5,000 katika kijiji hiki,” Diwani wa Kata ya Kebanchabancha, Philemon Matiko amewambia waandishi wa habari waliotembelea mradi huo, Machi 9, 2022.

Diwani Matiko akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)

Kwingineko katika kijiji cha Makundusi, RUWASA inasimamia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa tenki lenye uwezo wa kuchukua lita 90 kwa wakati mmoja na kusambaza maji kwa wananchi kupitia vituo 12.

Afisa Utumishi wa RUWASA Mkoa wa Mara, Stanley Sing'ira akifungulia maji katika mojawapo ya vituo vya mradi wa Makundusi

“Gharama ya mradi huu wa kijiji cha Makundusi ni shilingi milioni 400 na utahudumia wanakijiji zaidi ya 6,000,” Mhandisi Mchele amewaeleza waandishi wa habari.

Mwenyekiti wa kijiji cha Makundusi, Joseph Nyaikobe amesema mradi huo utawaondolea wanakijiji adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji kwenye mito na visima vya asili.

Wananchi na viongozi wilayani Serengeti wamemshukuru Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipatia wilaya hiyo mabilioni ya fedha kwa ajili ya kuwaboreshea huduma ya maji safi na salama.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dkt Vicent Mashinji na Mhandisi Mchele wametaja matatizo makubwa yanayoikabili miradi ya maji inayotekelezwa chini ya RUWASA wilayani hapo kuwa ni uharibifu wa miundombinu unaofanywa na wananchi wasio wema na ukosefu wa umeme wa kusukuma maji.

Dkt Mashinji

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages