TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Tarime mkoani Mara, leo Machi 23, 2022 imewafikisha katika Mahakama ya Wilaya hiyo watumishi wa umma wanne, kwa mashtaka ya rushwa na uhujumu uchumi.
Watumishi hao wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), ni Mhandisi Ernest Matakwali Maungo, John Fabian Nago (Fundi Sanifu), Mwalimu Victoria Sara Jonas (aliyekuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Manga) na Mwalimu Mukama Benedicto Mazigo (Afisa Elimu, Vifaa na Takwimu).
Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU na Mwanasheria wa Serikali, Mwinyi Yahaya amesoma mashitaka manne dhidi ya washtakiwa hao, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Tarime, Yohana Charles Myombo.
Mashtaka matatu (la kwanza hadi la tatu) yanawahusu washitakiwa wote, wakati shtaka la nne linamhusu Mhandisi Maungo pekee.
Mwendesha Mashtaka Yahaya ametaja shtaka la kwanza hadi la tatu kuwa ni matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri na la nne linalomkabili Mhandisi Maungo pekee ni ufujaji na ubadhirifu.
Hata hivyo, washtakiwa wote wamekana mashtaka hayo na wamepelekwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, hadi Aprili 6, 2022 watakaporejeshwa mahakamani hapo kwa ajili ya kusikilizwa kwa Shauri hilo Na. 10/2022.
Habari ya kina kuhusu mashtaka hayo itachapishwa kwenye toleo lijalo la gazeti la Sauti ya Mara.
(Imeandikwa na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment