NEWS

Wednesday 23 March 2022

Uchafuzi Mto Mara: LHRC, LEAT wataka ripoti za maji machafu mgodi wa North Mara ziwekwe hadharani, tume huru, NEMC ifumuliweKITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Chama cha Wanasheria wa Mazingira kwa Vitendo Tanzania (LEAT), vimetaka ripoti za usafishaji maji machafu katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara ziweke hadharani.

Sambamba na hilo, taasisi hizo zimetaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NECM) liundwe upya, lakini pia Makamu wa Rais aunde tume huru ya kuchunguza uchafuzi uliotokea mto Mara.

Hayo yamo kwenye taarifa kwa umma iliyotolewa leo Machi 23, 2022 kuhusu tamko la uchafuzi wa mto huo, iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Wakili Anna Henga na Mkurugenzi Mtendaji wa LEAT, Dkt Rugemeleza Nshala.

“LHRC na LEAT vinataka kuwasilishwa mara moja kwa ripoti za usafishaji maji machafu zitolewazo kila mwezi na North Mara Gold Mine ambayo mabwawa yake ya kuhifadhi maji machafu yako jirani na mto Mara na eneo lililochafuliwa.

“Kuundwa upya kwa Baraza la Usimamizi wa Mazingira nchini kutokana na kushindwa kwake kuchukua hatua stahiki za kupambana na uchafuzi wa mazingira katika eneo la mto Mara na nchini kwa ujumla,” imesema sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza:

“Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndiye Waziri halisi wa Mazingira nchini, aunde tume huru ya uchunguzi wa uchafuzi, ikijumuisha wanamazingira wanaoaminika na wenye weledi mkubwa wa kisayansi kutoka ndani na nje ya nchi.”

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya Kamati ya Watu 11 iliyoundwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo kuweka hadharani ripoti ya uchunguzi wa uchafuzi wa mto Mara, LHRC na LEAT zimefuatilia ili kujiridhisha na kuona namna wahanga husika wanaweza kusaidiwa.

Katika taarifa hiyo, LHRC na LEAT vimeeleza kutoridhishwa na ripoti ya Kamati ya Waziri Jafo iliyosema chanzo cha uchafuzi wa maji na vifo vya samaki vilivyotokea hivi karibuni mto Mara eneo la Kirumi darajani ni kinyesi cha ng'ombe, mkojo wa ng'ombe na uozo wa mimea.

“LHRC na LEAT vilifuatilia na kutembelea baadhi ya vijiji na vitongoji ambavyo vimeonekana kuathirika ili kubaini chanzo na athari zilizosababishwa na uchafuzi huo. Na kuanzia tarehe 17 hadi 20 Machi 2022 vilitembelea maeneo yanayozunguka na kutegemea huduma na matumizi ya maji katika mto Mara,” imeeleza sehemu nyingine ya taarifa hiyo.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages