NEWS

Monday 11 April 2022

Katibu CCM Tarime aonya viongozi wanaopanga safu na wanaoficha fomu za kugombea uongozi



KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Valentine Maganga (pichani), ametoa onyo kwa viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama hicho wilayani humo, wanaopanga safu za uongozi kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa viongozi wa chama hicho tawala.

Pia, Maganga amekemea tabia ya viongozi wanaoficha na kuwanyima baadhi ya wanachama wa CCM fomu za kugombea uongozi, akisema Chama hakitawaonea huruma watakaothibitika kutenda kosa hilo.

Katibu huyo ametaka wanachama waachwe huru waweze kutimiza haki yao ya kikatiba ya kugombea na kuchaguliwa.

“Ni marufuku kupanga safu kwa lengo lolote lile, waacheni wanachama watimize haki yao ya kikatiba… nakemea tabia ya kuficha fomu, kuwanyima baadhi ya wana-CCM fomu kwa visingizio vyovyote, kuendelea na tabia hiyo ni kosa kikanuni,” Maganga amesisitiza katika mazungumzo na Mara Online News ofisini kwake leo Aprili 11, 2022.

Amesema viongozi walio madarakani wakiwemo madiwani, wenyeviti wa vijiji, mitaa na wale wa jumuiya za CCM wana jukumu la kuhamasisha wanachama kugombea nafasi mbalimbali za chama hicho na jumuia zake.

Manganga ametumia nafasi hiyo pia kutoa wito wa kuhamasisha wana-CCM wote wenye sifa kujitokeza kuchukua fomu za kugombea bila woga, kwani nafasi za uongozi ndani ya chama hicho hazina hati miliki ya mtu yeyote.

“Nawaomba sana wana-CCM wote tuchukue fomu za kugombea bila kumuogopa mtu, nafasi zote zilizotangazwa kugombewa si mali ya mtu yeyote, gombea nafasi yoyote utakayoona inakufaa,” amesisitiza Katibu huyo wa CCM Wilaya ya Tarime.

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages