MELI ya kivita ya Urusi iliyoharibiwa na mlipuko juzi Jumatano imezama, Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema.
Kulingana na ujumbe wa wizara hiyo, meli hiyo inayoitwa Moskva, ilikuwa ikivutwa katika Bahari Nyeusi kwenda bandarini wakati "dhoruba" ilipoisababisha kuzama.
Meli hiyo ya kubeba makombora na wafanyakazi 510 ilikuwa ishara ya nguvu za kijeshi za Urusi, ikiongoza mashambulizi yake ya majini dhidi ya Ukraine.
Kyiv, Ukraine inasema makombora yake yaligonga meli hiyo ya kivita, ingawa Moscow, Urusi haijaripoti shambulio lolote. Inasema ilizama baada ya moto.
Moto huo ulisababisha mlipuko wa risasi za meli hiyo ya kivita, Urusi inasema na kuongeza kuwa wafanyakazi wote baadaye walihamishiwa kwenye meli za Urusi zilizokuwa karibu katika Bahari Nyeusi.
Baada ya kusema awali meli ya kivita ilikuwa inaelea, jana Alhamisi jioni vyombo vya habari vya Serikali ya Urusi vilitangaza kwamba Moskva ilikuwa imepotea.
"Wakati ikivutwa... kuelekea bandari iliyokusudiwa, meli hiyo ilipoteza usawa wake kutokana na uharibifu uliokuwa ndani ya meli wakati moto ulipozuka baada ya risasi kulipuka. Kutokana na hali ya bahari iliyochafuka, meli hiyo ilizama," Shirika la Habari la Serikali Tass lilinukuu Wizara ya Ulinzi ya Urusi.
Maafisa wa kijeshi wa Ukraine walidai kuwa waliipiga Moskva kwa makombora ya Neptune yaliyotengenezwa na Ukraine - silaha iliyoundwa baada ya Urusi kutwaa eneo la Crimea mwaka 2014, na tishio la majini kwa Ukraine katika Bahari Nyeusi liliongezeka.
Afisa Mkuu wa Ukraine alisema kuwa wafanyakazi 510 wangeweza kuwa ndani ya Moskva.
Katika siku ya kwanza ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine Februari 24, 2022, Moskva ilipata sifa mbaya baada ya kukitaka kikosi kidogo cha askari wa mpaka wa Kiukreni wanaotetea Kisiwa cha Snake katika Bahari Nyeusi kujisalimisha - ambapo kwa kumbukumbu walitangaza ujumbe wa kukataa.
Moskva ilijengwa katika enzi ya Soviet na ilianza huduma mapema miaka ya 1980. Meli hiyo iliwekwa chini katika mji wa Kusini mwa Ukraine wa Mykolaiv, ambao umeshambuliwa kwa bomu na Urusi katika siku za hivi karibuni.
Meli hiyo ya kusafirisha makombora hapo awali ilitumiwa na Moscow katika mzozo wa Syria, ambapo ilivipa vikosi vya Urusi nchini humo ulinzi wa majini.
Inaripotiwa kuwa ilikuwa na makombora 16 ya kuzuia meli ya Vulkan na safu ya silaha za kupambana na manowari pamoja na topedo.
Ikiwa shambulio la Ukraine litathibitishwa, Moskva yenye tani 12,490 itakuwa meli kubwa zaidi ya kivita kuzamishwa na nguza ya adui tangu Vita ya Pili ya Dunia.
Ni meli ya pili kubwa ambayo Urusi imepoteza tangu kuanza kwa uvamizi wake.
Machi 2022, meli ya kutua ya Saratov iliharibiwa na shambulio la Ukraine katika bandari ya Berdyansk kwenye Bahari ya Azov ya Kiukreni iliyotekwa na Urusi. Chanzo: BBC
No comments:
Post a Comment