NEWS

Monday 11 April 2022

Mkurugenzi wa Professor Mwera Foundation ahamasisha mafunzo ya ufundi kwa vijana, walimuMKURUGENZI wa Taasisi ya Professor Mwera Foundation (PMF), Hezbon Peter Mwera (aliyesimama pichani juu), amehamasisha walimu kuchangamkia ofa inayotolewa katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime.

Hezbon alitoa hamasa hiyo katika kikao cha wakuu wa shule za sekondari za serikali na binafsi kutoka mikoa ya Mara, Mwanza na Geita, kilichofanyika ukumbi wa TTC mjini Tarime, Jumatano iliyopita.

“Tunawatangazia walimu ofa ya kuja kusoma fani yoyote ya ufundi inayotolewa katika chuo chetu bure. Hizi fani za ufundi ni muhimu, sio tu kwa vijana, bali hata kwa walimu,” alisema.

Alifafanua kuwa mafunzo ya ufundi yatawaongezea walimu ujuzi wa ziada unaoweza kuwasaidia kujiongezea kipato wakati wa likizo na wanaporudi nyumbani kutoka kufundisha wanafunzi shuleni.


Mkurugenzi Hezbon (kushoto) akizungumza kikaoni

Hezbon ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Kanda ya Ziwa, alitumia nafasi hiyo pia kuwaomba wakuu hao wa shule kumsaidia kuhamasisha vijana wa kike na kiume, wakiwemo waliohitimu kidato cha nne, kujiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime.

Alitaja fani zinazotolewa katika chuo hicho kuwa ni pamoja na ufundi umeme, magari, udereva, ushonaji na kompyuta.

“Vijana waliopata daraja la nne na alama sifuri wana fursa ya kujiunga na vyuo vya ufundi ili wasijione wametengwa… kupitia vyuo vya ufundi wanaweza kupanda hadi chuo kikuu na hatimaye kuajiriwa, au kujiajiri kutokana na fani walizosoma,” Hezbon alisema.

Kwa upande mwingine, Hezbon alisema Taasisi ya PMF pia imeidhinishwa na serikali kuendesha programu ya mafunzo ya kitaaluma kwa wafanyakazi wa sekta za hoteli na utalii katika mikoa 10.

“Mikoa hiyo ni Mara, Mwanza, Shinyanga, Kagera, Geita, Simiyu, Kigoma, Katavi, Rukwa na Ruvuma,” alisema Hezbon ambaye pia ni mmoja wa wanachama wa chama tawala - CCM waliotia nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Tarime Mjini kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2020.

Awali, akifungua kikao hicho, Afisa Elimu Mkoa wa Mara, Mwalimu Benjamin Oganga aliwataka wakuu wa shule kujenga utamaduni wa kuwamotisha walimu na wanafunzi katika shule zao.


Mwalimu Oganga (aliyesimama) akifungua kikao hicho

“Jengeni hamasa kwa walimu mnaowasimamia na wanafunzi, wajengeeni ari na moyo wa kupenda kufanya kazi nzuri,” alisisitiza Mwalimu Oganga ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mara Kitengo cha Elimu.

Aidha, aliwataka viongozi hao kuonesha mfano mzuri katika kusimamia uadilifu na nidhamu kwa walimu na wanafunzi.

Kikao hicho kilitanguliwa na kikao cha wakuu wa shule za sekondari za mkoani Mara kilichofanyika kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Tarime inayomilikiwa na Taasisi ya Professor Mwera Foundation.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwalimu Oganga aliishukuru Taasisi ya PMF na kuitaja kama mdau mkubwa wa elimu anayestahili kuungwa mkono na viongozi wa elimu na serikali kwa ujumla katika juhudi za kuhamasisha elimu na mifumo ya kitaaluma.


Mwalimu Oganga (kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi Hezbon mara baada ya ufunguzi wa kikao cha Jumatano iliyopita.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages