NEWS

Monday 11 April 2022

Waziri Chana awaalika Watanzania maadhimisho ya miaka 100 ya urithi wa Mwalimu Nyerere wilayani Butiama



WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt Pindi Chana (pichani), amewahimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho ya kusherehekea miaka 100 ya Urithi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yatakayofanyika Aprili 13, 2022 Butiama mkoani Mara, ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Akizungumza jijini Dodoma leo, Balozi Dkt Chana amesema lengo la maadhimisho hayo yanayoandaliwa na Wizara hiyo kwa kushirikiana na mkoa wa Mara na wadau mbalimbali, ni kuenzi na kusherekea mchango maridhawa alioutoa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere katika Nyanja mbalimbali kitaifa na Kimataifa.

Amesema maadhimisho hayo ni sehemu ya kutekeleza mpango wa miaka 10 wa kuenzi urithi wa maisha ya Rais huyo wa Kwanza Tanzania, unaolenga kuwashirikisha wadau kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mchango wake na umuhimu wa kumuenzi, kukusanya, kuendeleza, kuhifadhi na kutangaza rasilimali za urithi wake kwa manufaa ya kiazi cha sasa na vijavyo ili kukuza na kuedeleza utalii.

“Tarehe 13 Aprili, 1922 ndiyo siku aliyozaliwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kama angekuwa hai tarehe 13 Aprili, 2022 angetimiza miaka 100, hivyo tunasherehekea kuenzi Urithi wa maisha ya Hayati Baba wa Taifa,” amesisitiza Waziri Chana.

Waziri Chana amewaalika wananchi na wadau mbalimbali, wakiwemo waandishi wa habari kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.

“Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na mkoa wa Mara tunawaalika wananchi na wadau wote kushiriki kwenye kilele cha maadhimisho haya, vilevile kuendelea kuenzi kwa vitendo Urithi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa letu,” amesema.

Ameongeza kuwa kuelekea kilele cha maadhimisho hayo, matukio mbalimbali yanaendelea kufanyika ikiwa ni pamoja na mikutano ya wadau mbalimbali, mashindano ya baiskeli, matembezi ya hiari na midahalo inayoendeshwa na taasisi tofautii.

Pia, amesema wakati wa kilele cha maadhimisho hayo kutakuwa na burudani mbalimbali, programu za wanafunzi za kielimu, uzinduzi wa Mpango wa Kuenzi Urithi wa Mwalimu Nyerere, nembo maalum ya Mwalimu@100 na onesho maalum la Mwalimu Nyerere.

(Na Mwandishi wa Mara Online News, Dodoma)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages