NEWS

Tuesday 12 April 2022

Mfanyakazi bora Taasisi ya Professor Mwera Foundation apewa tuzo, walimu wapewa zawadiTAASISI ya Professor Mwera Foundation (PMF) imemtambua mfanyakazi wake bora kwa kumpa tuzo iliyoambatana na fedha taslimu.

Pia, imewapa zawadi za fedha taslimu walimu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Tarime inayomilikiwa na taasisi hiyo, ambao masomo yao yalipata alama A na B katika mitihani ya taifa ya kidato cha pili na cha nne mwaka 2021.

Aliyekabidhi tuzo hiyo na zawadi hizo kwa washindi katika hafla iliyofanyika shuleni hapo leo Aprili 12, 2022, ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo, Askofu Paul Baru.

Mfanyakazi bora aliyetwaa tuzo hiyo ni Mlezi wa shule hiyo, Ester Richard (pichani juu), huku walimu Collins Matonye, Madame Kalinga, Andrew Andrew, Simion Makala, Nyasebwa James na Maria Daniel wakijinyakulia zawadi za fedha taslimu kwa viwango tofauti.Wakati hafla hiyo ikiendelea, Mwasisi wa PMF, Peter Mwera, alipiga simu kupitia kwa Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Hezbon Peter Mwera, kuwapongeza washindi wa tuzo na zawadi hizo na kuwataka kuongeza bidii na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao.Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi huyo wa PMF, amesema wataendelea kutoa tuzo kwa wafanyakazi, wanafunzi na walimu wa sekondari hiyo na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime ambacho pia kinamilikiwa na taasisi hiyo.

“Tutakuwa tunatoa tuzo ya mfanyakazi bora wa Taasisi ya Professor Mwera Foundation kila baada ya miezi mitatu, tutafanya hivyo pia kwa wanafunzi, wanachuo na walimu bora,” amesema Hezbon.
Askofu Baru (kulia) naye alikabidhiwa zawadi na Meneja Uendeshaji wa Taasisi ya PMF, Mwalimu Mwita Samson Marwa katika hafla hiyo.

Mwaka jana, taasisi hiyo ilizipatia shule bora mkoani Mara tuzo zenye thamani ya shilingi milioni 12, kwa kukishirikiana na ofisi za Afisa Elimu na Mkuu wa Mkoa.

“Pia, hivi karibuni tumetoa tuzo kwa shule bora mkoani Shinyanga na sasa hivi tunajiandaa kutoa kwenye mikoa ya Mara, Simiyu na Geita, lakini pia tutatoa tuzo kwa Wakuu wa Shule za Sekondari Kanda ya Ziwa,” amesema Mkurugenzi huyo wa PMF.

Hezbon ametumia nafasi hiyo pia kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ya kuiletea nchi maendeleo, yakiwemo ya kielimu.

“Ninamshukuru na kumpongeza Mama [Rais Samia] kwa kufungua mipaka na kuleta fursa nyingi kwa Tanzania na kuendeleza mambo mazuri yaliyoanzishwa na mtangulizi wake, Dkt John Pombe Magufuli.

“Nampongeza Rais wetu pia kwa maono makubwa ya kuondoa ujinga, umaskini na maradhi. Tunaona juhudi zake katika shule - anatoa fedha za kujenza madarasa ili kuongeza fursa kwa watu wengi kupata elimu,” amesema Hezbon ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Kanda ya Ziwa.

Ameongeza kuwa Rais Samia pia anastahili pongezi kwa kuonesha dhamira ya kuanzisha vyuo vya ufundi kila wilaya nchini. “Vyuo hivi vitasaidia vijana wengi waliohitimu kidato cha nne, kukata tamaa na kuzurura mitaani kutokana na kukosa ajira,” amesema.


Mkurugenzi Hezbon (katikati) akizungumza katika hafla hiyo

Kwa upande mwingine, Hezbon ametoa wito kwa wamiliki na wakuu wa vyuo vya ufundi nchini kutoa fursa kwa vijana na kuwahamasisha kujiunga na vyuo vya ufundi.

Amewaomba pia wanapopata nafasi wasisite kusaidia vijana yatima na wanaoishi katika mazingira magumu kupata elimu ili waweze kufikia malengo yao ya kimaisha.

“Lakini pia, ninawaomba waliobarikiwa kuwa na uwezo wa kiuchumi waanzishe miradi ya kusaidia jamii kuondokana na ujinga, umaskini na maradhi.

“Tunapokuwa tunapiga hatua ya maendeleo kwa pamoja, inakuwa ni jambo la faraja na la heri sana kuliko kufanya maendeleo ya mtu mmoja mmoja, au watu wachache wachache,” amesisitiza Hezbon.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages