NEWS

Tuesday 5 April 2022

Rais Samia afungua mkutano wa Kituo cha Demokrasia Tanzania, ataja siri ya kuijenga nchiRAIS Samia Suluhu Hasaan (pichani) amesema ustawi wa Tanzania hautajengwa kwa utengano wa watu, au vyama vya siasa.

“Tanzania haitajengwa na mtu mmoja, haitajengwa na chama kimoja. Nchi hii itajengwa na wote. Wote kama Watanzania lazima tujadili mambo yetu... lazima tujadili wote kama Watanzania,” Rais Samia amesisitiza hayo leo Aprili 5, 2022 wakati akifungua mkutano wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) unaojadili maridhiano, haki na amani, unaofanyika jijini Dodoma.

Ameongeza “Tulichagua kuingia mfumo huu wa vyama vingi tukijua kwamba ndani ya mfumo huu tutakwenda kupata maendeleo ya haraka kwa sababu vyama viko vingi, macho yako mengi, maono yapo mengi.

“Tukikubaliana, tunakwenda kutekeleza wote kama Watanzania. Atakayekiuka hapo, ni mkosaji – awe ametoka kokote kule… hiyo ndio itakayokwenda kutuongoza katika utendaji wetu na maisha yetu.”

Mkuu huyo wa nchi amesisitiza kuwa maendeleo ya Tanzania yanahitaji mchango wa kila Mtanzania, akitolea mfano zabuni za miradi inayotekelezwa kutokana na fedha za UVIKO-19, ambazo zimegawanywa kwa wakandarasi wazawa bila kuangalia itikadi zao za kisiasa.

Aidha, Samia amesema Serikali ya Awamu ya Sita anayoiongoza itaendelea kutoa kushirikisha makundi mbalimbali ya Watanzania katika masuala yenye maslahi mapana ya Taifa. “Ushirikishaji kutoka serikalini ni wa uhakika,” amesema.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages