NEWS

Tuesday 5 April 2022

Wabunge waipiga chini ripoti ya Jafo kuhusu uchafuzi wa Mto Mara, Profesa Muhongo ataka isiwekwe kwenye tovuti ya Serikali



WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo Aprili 5, 2022 wameikataa ripoti ya uchunguzi wa uchafuzi wa maji na vifo vya samaki katika Mto Mara, wakisema ni ya upotoshaji na inayoitia aibu nchi mbele ya uso wa dunia.

Ripoti hiyo ni ile iliyoandaliwa na Kamati ya Kitaifa ya watu 11 iliyoongozwa na Profesa Samweli Mayele, ambayo iliundwa na Waziri mwenye dhamana ya mazingira, Selemeni Jafo (pichani juu).

Baada ya ripoti hiyo kuwasilishwa bungeni, wabunge 18 wameipinga na kutaka iundwe tume huru ya kuchunguza uchafuzi huo, huku miongoni mwao akiwemo Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo wakiomba isiwekwe kwenye tovuti ya Wizara kwani inafedhehesha na haina afya kwa Taifa.

"Ripoti ya Kamati ya Kitaifa kuhusu uchafuzi wa Mto Mara ina upotoshaji, isiwekwe hata kwenye tovuti ya Wizara, hakuna mafuta Ziwa Victoria, kwanza ikiwekwa kwenye tovuti, UNESCO watanishangaa mimi mtaalamu wa eneo hili," amesema Profesa Muhongo.

Mbunge wa Viti Maalum, Neema Rugangira amehoji kwamba kama uchunguzi ulikuwa unahusisha mambo ya vyakula, ilikuwaje mamlaka nyingine husika kama vile Wizara ya Afya na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) hazikushirikishwa.

Pia amehoji ni kwanini awali ripoti ilisema kinyesi na mikojo ya mifugo kuwa ndiyo chanzo cha uchafuzi wa maji na vifo vya samaki, lakini leo imesema chanzo ni mvua kubwa.

“Kingine lazima tujue watu wa NEMC ni kwanini mmeshindwa kuzuia bwawa la maji machafu katika mgodi wa North Mara ambalo sheria inasema lisizidi maji lita 800,000 lakini ninyi mmeruhusu hadi lita milioni 2.5 halafu mnasema vitu ambavyo haviingii akilini,” amesema Mbunge wa Viti Maalumu, Jeska Kishoa.

Kutokana na kutoridhishwa na ripoti hiyo, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma ametangaza kujiuzulu nafasi ya ubalozi wa mazingira nchini.

Kwa upande wake, Waziri Jafo amesema kuna mambo mengi ambayo yakisomwa kwenye ripoti yatawapa mwanga wabunge.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages