NEWS

Friday 8 April 2022

Watanzania kusherehekea miaka 100 ya Mwalimu Nyerere Butiama


WATANZANIA wanaelekea kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Sherehe za maadhimisho hayo zitafanyika kitaifa Aprili 13, 20202 kwenye viwanja vya Mwenge kijijini Butiama, yalipo Makumbusho ya Mwalimu Julius K. Nyerere.

“Hii ni sherehe ya kufurahia maisha ya Baba wa Taifa, kwa sababu licha ya kwamba hayuko hai, bado mawazo, falsafa na mitazamo yake kwa taifa vinaishi,” Mkurugenzi wa Makumbusho hiyo, Emmanuel Kiondo amewambia waandishi wa habari ofisini kwake leo.

"Mwalimu Nyerere angekuwa hai mwaka huu angekuwa anatimiza miaka 100 tangu kuzaliwa kwake na hili tukio ni tofauti na lile la kumbukumbu ya kifo chake linaloadhimishwa Oktoba 14 kila mwaka," Kiondo amesema. 

Amesema Makumbusho ya Mwalimu Julius K. Nyerere Butiama yanaandaa onesho la kipekee lililosheneni historia ya Rais huyo wa kwanza Tanzania. “Onesho hilo litakuwa na vitu vizuri sana,” amesisitiza.


Kiondo (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari ndani ya Makumbusho ya Mwalimu Julius K. Nyerere yaliyopo Butiama.

Kiondo amesema sherehe hizo zina maana kubwa kwani misingi iliyowekwa na Mwalimu Nyerere imeendelea kuheshimiwa, kusimamiwa na kutekelezwa na viongozi wa nchi kwa vitendo.

“Viongozi wote wa serikali wanapita kwenye misingi iliyowekwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, mfano Azimio la Musoma lililohamasisha elimu kwa wote, marais wote wanalitekeleza,” amefafanua.

Kulingana na Mkurugenzi Kiondo, tayari Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeanza kuratibu mpango wa miaka 10 wa kumuenzi Mwalimu Nyerere, utakaohusisha wadau kutoka sekta mbalimbali.

Amesema kilele cha sherehe hizo kitatanguliwa na maonesho maalumu ya siku tatu [Aprili 11 – 13, 2022] kuhusu namna misingi iliyowekwa na Mwalimu Nyerere inavyotekelezwa katika taasisi tofauti, bila kuweka kando burudani mbalimbali.

Mkuu wa Wilaya (DC) ya Butiama, Mwalimu Moses Kaegele amesema maandalizi ya sherehe za maadhimisho hayo yanaendelea vizuri na amewakaribisha Watanzania kujitokeza kwa wingi kuadhimisha tukio hilo la kumuenzi Baba wa Taifa.

DC Kaegele amesema maadhimisho hayo yatahusisha pia shughuli za upandaji miti katika taasisi za umma, ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Butiama kama sehemu ya kuenzi falsafa ya kulinda na kutunza mazingira iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere.


DC Kaegele akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika viwanja vya Makumbusho ya Mwalimu Julius K. Nyerere - Butiama.

Pia Mkuu huyo wa wilaya ametoa wito wa kuwahimiza wakazi wa Butiama kujiandaa vizuri kwa ajili ya mapokezi mazuri ya wageni na kutoa huduma za kibiashara.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo yenye kaulimbiu inayosema “Mwalimu Julius Kambarage Nyerere @100, Tumuenzi kwa Kudumisha Umoja, Amani, Uhuru na Kazi.”

Baba wa Taifa, Mwalimu Julus Kambarage Nyerere alizaliwa Aprili 13, 1922 kijijini Butiama katika mkoa wa Mara na alifariki dunia Oktoba 14, 1999 nchini Uingereza wakati akipata matibabu, kisha mwili wake ulirejeshwa Tanzania na kuzikwa nyumbani kwake Mwitongo, Butiama.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages