NEWS

Tuesday 31 May 2022

Baraza la Madiwani Tarime Mji lafutilia mbali majina ya mitaa na barabara yaliyowekwa ‘kijanjajanja’BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Tarime limeazimia kufutilia mbali majina yasiyo na hadhi ya kutumika katika mitaa na barabara za mji huo.

Azimio hilo limeungwa mkono na Mkurugenzi, Gimbana Ntavyo katika kikao maalum cha maamuzi, kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Daniel Komote mjini Tarime, leo Mei 31, 2022.

Miongoni mwa majina yaliyofutwa ni Gimunta na Ghati Matunda, ambayo imethibitika yaliwekwa ‘kijanjajanja’ kwenye vibao vya mitaa na barabara za mji huo, baada ya kufutwa kwa majina ya watu na vitu maarufu.

Mwenyekiti Komote (kushoto) na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Ntavyo, wakiwa kikaoni leo.

Baada ya kupitisha azimio hilo, Komote ameitaka Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Tarime kuweka vibao vya majina ya watu maarufu na waasisi wa maeneo husika ili kuziba nafasi za yaliyofutwa katika mitaa na barabara za mbalimbali.

Awali, katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichopita, Mwenyekiti Komote ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nkende, alikemea hujuma iliyofanyika ya kufuta majina ya watu na vitu maarufu na kuweka yasito na hadhi ya kuwekwa kwenye vibao vya barabara na mitaa katika mji huo.

“Haiwezekani ufute majina ya Uhuru na Kawawa. Nani asiyemjua Kawawa hapa nchini na duniani kote? Hiwezekani ufute jina la NMB - tumezaliwa benki ikiwa pale, haiwezekani ufute majina ya Sokoine, Zambia, Samora Machelle, Starehe na Migombani.

“Mmefuta majina ya waasisi wa nchi hii mmeweka ya kwenu. Mmeleta taharuki mjini, mmeondoa majina original (ya asili), tunataka yarudi. Mnaweka majina ambayo hayana hata historia, tumeelekeza kwamba ni lazima vibao hivyo viondolewe mara moja ndani ya siku mbili,” alisema Komote.

Naye Diwani wa Viti Maalum, Nuru Hotai alilaani kitendo cha kuacha majina ya viongozi maarufu, akiwemo Hayati Dkt John Pombe Magufuli na kuweka ya wasio na umaarufu.

“Nilitegemea jina la Magufuli lipate barabara, au mtaa maana hata soko la kisasa tunalolijenga Magufuli alihakikisha tunalipata, lakini kwenye yale majina yote jina lake halimo, kweli jamani,” alisema Nuru.
(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages