NEWS

Thursday 26 May 2022

Finland, UNFPA waunganisha nguvu kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa wasichana wenye ulemavu wilayani Tarime kupitia ATFGM MasangaMKUU wa Ushirikiano katika Ubalozi wa Finland nchini Tanzania, Dkt Timo Voipio amesema wasichana wakiwemo wenye ulemavu, wana mchango katika ujenzi wa taifa, endapo watawezeshwa na kulindwa dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.

Dkt Voipio amesisitiza hayo wakati wa ziara yake na maofisa wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Afya ya Uzazi (UNFPA) ya kukagua utekelezaji wa mradi wa Chaguo Langu Haki Yangu katika Shirika la ATFGM Masanga wilayani Tarime, jana Mei 25, 2022.

“Jamii inapaswa kuachana na mila zilizopitwa na wakati ikiwemo ukeketaji, kwani ni ukatili na unyanyasaji wa kijinsia - ambao huchangia kumnyima mtoto wa kike haki ya kupata elimu,” amesema Dkt Voipio.


Dkt Timo Voipio (kushoto) katika picha ya pamoja na Debora (katikati) na Bhoke waliopata usaidizi wa kielimu katika Shirika la ATFGM Masanga.

Kwa mujibu wa Meneja Mawasiliano wa UNFPA, Warren Bright, Chaguo Langu Haki Yangu ni programu ya miaka mitatu na nusu (2021-2025), inayotekelezwa na shirika hilo kwa kushirikiana na Ubalozi wa Finland nchini Tanzania.

Bright amesema malengo ya programu hiyo ni kuhakikisha kuwa haki na fursa za kuchagua kwa wanawake na wasichana, hususan wenye ulemavu zinalindwa na kuimarishwa kupitia mwitikio wa sekta mbalimbali unaokabili unyanyasaji wa kijinsia na mila kandamizi, ikiwemo ukeketaji na ndoa za kulazimishwa katika umri mdogo.


Kiongozi kutoka UNFPA (kulia) akisoma mabango yaliyooneshwa na wasichana wanaohudumiwa na Shirika la ATFGM Masanga wakati wa ziara hiyo.

Wanufaika wa moja kwa moja wa programu hiyo, kwa mujibu wa UNFPA, ni wasichana walio katika rika balehe na wasichana vijana, hususan wanawake na wasichana wenye ulemavu wanaoishi katika mikoa ya Shinyanga (wilaya ya Kishapu na Kahama), Mara (Tarime na Butiama) na Zanzibar (Mjini Unguja na Chake Chake, Pemba) walio hatarini, au waathirika wa ukatili wa kijinsia, hasa ukeketaji na ndoa za utotoni.

“Programu hii ni sehemu ya utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto (NPA-VAWC) Tanzania Bara (2016/17-2021/22) na Zanzibar (2017-2011),” amesema Bright.


Warren Bright akizungumzia programu ya Chaguo Langu Haki Yangu

Naye Meneja Miradi wa ATFGM Masanga, Valerian Mgani amesema utekelezaji wa programu ya Chagu Langu Haki Yangu utahamasisha uimarishaji wa miundombinu iliyowekwa na Serikali na kutoa elimu ya madhara ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, hasa kwa watoto wakiwemo wasichana wenye ulemavu.

“Utekelezaji wa mradi huu pia utasaidia kuunganisha walengwa wa mradi kwenye mtandao wa kitaifa wa watu wenye ulemavu kwa ajili ya msukumo wa kupata haki na mahitaji yao,” amesema Mgani.


Valerian Mgani (kulia) akizungumza wakati wa ugeni huo kutoka Finland na UNFPA

Shirika la ATFGM Masanga limejikita katika utoaji wa elimu ya madhara ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, ikiwemo ukeketaji, vipigo, ndoa na mimba za utotoni.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages