NEWS

Thursday 26 May 2022

Fisi waua mwananchi Tarime Vijijini



MWANAUME aliyetambuliwa kwa jina la Moseti Marwa, ameuawa kwa kushambuliwa na fisi katika kijiji cha Kangariani wilayani Tarime, Mara.

Taarifa zilizotufikia hivi punde zinasema kundi la fisi limemshambulia na kumtafuna sehemu mbalimbali za mwili na kubakiza vipande vya mifupa.

Inaelezwa kuwa mwanakijiji huyo ameshambulia juzi usiku akiwa anatembea kwa miguu kuelekea nyumbani kwake.

“Tunavyoona fisi wale walikuwa zaidi ya mmoja, maana walikula hadi kichwa,” Katibu Mwenezi wa Chama tawala - CCM Kata ya Itiryo, Gibuka Motera ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu, leo asubuhi.

Mazishi ya marehumu huyo yamefanyika jana Jumatano na kuhudhuriwa pia na Diwani wa Kata ya Itiryo, Shadrack Marwa (CCM).

“Tukio hili lilitokea usiku wa juzi, na huyu mtu alikuwa bonge lakini tumezika fuvu tu, wametafuna kila kitu,” amesema Diwani Marwa.

Inadaiwa fisi ambao haijulikani walikotokea wanazunguka katika kata hiyo na maeneo jirani, hivyo kuleta hofu kwa wananchi.

Baadi ya vijiji vya wilaya ya Tarime vinapakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages