NEWS

Monday 30 May 2022

Mwanaume aliyeua mke wake kikatili kwa kummiminia risasi asakwa kila konaJESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza, linamsaka mwanaume aliyemuua mke wake kikatili kwa kumpiga risasi kadhaa.

Salha Salum (26), mkazi wa Buswelu wilayani Ilemela, Mwanza, ameuawa kwa kupigwa risasi sehemu mbalimbali mwilini.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ofisa Mnadhimu, Gidion Msuya amewambia waandishi wa habari jijini Mwanza jana kwamba Salha alifikwa na mauti hayo Mei 28, mwaka huu, saa 2:30 usiku nyumbani kwake.

Inadaiwa kuwa Salha na mumewe walifunga ndoa mapema mwaka huu kuelekea mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Msuya amesema mwanaume ambaye jina lake halijafahamika, anadaiwa kumuua mke wake huyo kwa kummiminia risasi zaidi ya moja mwilini na kusababisha kifo chake papo hapo.

Amesema chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi zaidi.

Ameongeza kuwa baada ya mauaji hayo, mwanaume huyo alikimbilia kusikojulikana, hivyo askari polisi wanamsaka ili kumfikisha kwenye vyombo vya sheria.

"Tukio hilo lipo, linahusisha wanandoa wawili (mke na mume), mtuhumiwa anatafutwa baada kutoroka na tunachunguza chanzo cha mauaji, ingawa taarifa za awali zinaeleza kuwa ni wivu wa mapenzi," amesema Msuya.

Kaimu Kamanda huyo wa Polisi amesema mtuhumiwa huyo alitekeleza mauaji hayo kwa kutumia bastola.

(Na Mwandishi wa Mara Online News, Mwanza)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages