NEWS

Monday 30 May 2022

Wamarekani wachangishana mamilioni kuendeleza Kituo cha Maarifa cha Madaraka Nyerere wakipanda Mlima KilimanjaroSHIRIKA la Tanzania Development Support (TDS) la nchini Marekani, limetoa msaada wa Dola za Kimarekani 33,000 (sawa na shilingi milioni 76.5), kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kielimu katika Kituo cha Maarifa cha Madaraka Nyerere kilichopo Sekondari ya Nyegina wilayani Musoma, Mara.

Mwenyekiti wa Bodi ya Uendeshaji wa Kituo hicho, Madaraka Nyerere amesema kituoni hapo juzi kwamba fedha hizo zimetokana na baadhi ya wana-TDS kuja nchini na kupanda Mlima Kilimanjaro, ikiwa ni sehemu ya shughuli walizofanya kuhamasisha marafiki na jamaa zao kuchangia uendelezaji wa kituo hicho.

Madaraka amesema kituo hicho siyo mali yake binafsi, bali kilipewa jina hilo kufuatia ombi la Mama yake, Maria Nyerere, baada ya kuombwa kiitwe kwa jina lake kwa sababu aliwahi kufundisha kwenye shule hiyo.

“Alisema [Mama Maria Nyerere] kwa kuwa amezeeka na mimi ndiye hushirikiana na wana-TDS kupanda Mlima Kilimanjaro ili kuchangisha fedha za kuendeleza kituo hiki, aliomba kiitwe kwa jina langu,” amesema Madaraka ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Madaraka Nyerere (aliyesimama) akizungumza katika hafla hiyo

Mmiliki wa kituo hicho na Sekondari ya Nyegina ni Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma, ambaye mwaka jana waliingia mkataba na TDS kukiendeleza kwa miaka mitano na baadaye majukumu hayo yatakabidhiwa kwa mmiliki.

Shughuli zinazotekelezwa na kituo hicho ni pamoja na maktaba za vitabu na kompyuta, mradi wa kuandaa watoto kabla hawajaanza shule ya msingi na mpango wa kuelimisha walimu kazini, ambapo mwaka huu wamedhamiria kuwezesha walimu kuboresha matumizi ya lugha ya Kiingereza.

Shirika la TDS pia linafadhili wanafunzi 10 wa kike katika kila darasa kwa asilimia 100.

Akizungumza kwa niaba ya wazazi wa watoto wanaofadhiliwa na TDS, Christian Costantine amesema ufadhili huo umekomboa watoto wa kike kielimu katika eneo hilo.

Wanafunzi wa Kituo cha Maarifa cha Madaraka Nyerere

“Kila mwanafunzi anayefadhiliwa analipiwa ada yote shilingi milioni 1.5, sare, pedi (taulo za kike), sabuni na mahitaji yote muhimu ya shuleni. Kwa kweli wazazi tunakosa maneno yanayotosha kuwasilisha shukrani tulizonazo kwa TDS,” amesema Costantine.

Pia, ameupongeza uongozi wa kituo hicho, akisema mfumo unaotumika kupata watoto wa kufadhiliwa hauna upendeleo, unawezesha kupata walengwa ambao wanakuwa na uwezo mkubwa kitaaluma, lakini wanaotoka katika familia zisizojiweza kiuchumi.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages