NEWS

Sunday 29 May 2022

Halmashauri ya Serengeti yaanza kupaa, yajayo yanafurahisha zaidiHALMASHAURI ya Wilaya ya Serengeti imeanza kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, baada ya kupitia kipindi kigumu cha mlipuko wa janga la UVIKO-19.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ayub Mwita Makuruma (pichani juu aliyesimama), ameyasema katika hotuba yake kuahirisha kikao cha Baraza la Madiwani mjini Mugumu, jana Ijumaa.

Makuruma amesema tayari hamashauri hiyo imetoa shilingi milioni 400 kwa ajili ya kughamiria miradi ya maendeleo ya wananchi katika mwaka huu wa fedha (2021/2022) kutokana na mapato ya ndani.

“Kitakwimu tupo vizuri kwenye mapato ya ndani kwa sasa. Shilingi milioni 400 zimepelekwa kwenye miradi ya maendeleo,” Makuruma amesema katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa pia na viogozi mbalimbali, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dkt Vincent Mashinji na Mbunge wa Serengeti, Amsabi Mrimi.

Amesema hakmashauri hiyo inatarajia kupeleka Sh takriban milioni 500 kugharimia miradi ya maendeo ili kubosresha huduma za jamii kwa wananchi kufikia mwisho wa mwaka huu wa fedha.

Baadhi ya madiwani kikaoni

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, halmashauti hiyo ilikuwa haifanyi vizuri katika kukusanya mapato na kwamba hali ilikuwa mbaya zaidi kipindi cha COVID-19.

“Watu wanasahau tulikotoka, kipindi cha nyuma hakuna fedha ilikuwa inaenda kwenye miradi kutoka kwenye asilimia 40, mapato yalikuwa yanapotea,“ amesema Makuruma huku akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Kivuna Msangi kwa kusimamia vizuri suala la utendaji kwa kipindi kifupi ambacho amehudumu.

Ameongeza kuwa hata fedha za vikundi vya wanawake, vijana na wenye lemavu, sasa zimeanza kutolewa na halmashauri hiyo bila tatizo.

Aidha, amesema Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeipatia halmashauri hiyo Sh zaidi ya bilioni saba kugharimia miradi mbalimbali ya maendeleo. Ametumia fursa hiyo pia kumshukuru Rais Samia kwa kujali maendeleo ya wananchi.

Mwenyekiti huyo amesema ujio wa Filamu ya Royal Tour utasadia kuongeza mapato ya ndani ya hamashauri hiyo kutokana na kodi zinazolipwa na wawekezaji katika sekta ya utalii wilayani hapa.

Rais Samia (aliyevaa ushungi) akishiriki katika uandaaji wa Filamu ya Royal Tour

Makuruma amesema watalii wameanza kumiminika katika hoteli na kambi za kitalii zizopo wilayani Serengeti.

“Kuna taarifa njema kuwa wageni wameanza kuwa wengi katika hoteli na camps (kambi) zilizopo Serengeti baada kuzinduliwa kwa Filamu ya Royal Tour,” Makuruma amesema huku akimpongeza Rais Samia kwa kuwapatia Watanzania zawadi ya filamu hiyo.

Makuruma amewataka madiwani wa halmashuri hiyo kuendelea kuisemea Serikali mambo mazuri inayofanya kwa wananchi na kuendelea kutumikia wananchi kwa moyo mkunjufu ili iweze kusonga mbele kimaendeleo.

“Serengeti ni yetu sote, tuitumikie kwa moyo mmoja,“ amesisitiza Makuruma ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Busawe kwa tiketi ya chama tawala - CCM.

Awali, Mweka Hazina mpya wa Halmashauri hiyo, Saad Ishabailu alijitambulisha kwenye kikao hicho na kutumia nafasi hiyo pia kuwaomba madiwani ushirikiano, hasa wa kumsaidia katika suala la ukusanyaji wa mapato ili kufanikisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya wananchi.

Mweka Hazina, Saad Ishabailu

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages