NEWS

Wednesday 22 June 2022

Mradi wa mamilioni ya fedha za UVIKO-19: RUWASA yashusha shehena ya mabomba ya kusambaza maji RoryaWAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) imepokea shehena ya mabomba yatakayotumika kusambazia maelfu ya wananchi wa wilaya ya Rorya huduma ya maji safi kutoka Ziwa Victoria.

Mabomba hayo yatatumika kutekeleza mradi wenye thamani ya shilingi milioni 630, chini ya Kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Mkuu wa Wilaya (DC) ya Rorya, Juma Chikoka ameongoza mapokezi ya mabomba hayo leo Juni 22, 2022 katika kijiji cha Raranya, nje kidogo ya makao makuu ya wilaya hiyo yaliyopo eneo la Ingiri Juu.

“Jambo la kwanza ni kuhakikisha wananchi wa Raranya wanapata maji, badaye yangie Ingiri [akimanisha makao makuu wa wilaya hiyo],” Chikoka amesema mbele wa wananchi waliojitokeza kushuhudia mapokezi ya mabomba hayo.

Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha upatikanaji wa mamilioni ya fedha hizo za UVIKO-19, ambazo alisema zimefanya kazi kubwa wilayani Rorya.

“Leo ni siku ya kipekee, mabomba haya yatasaidia kufikisha huduma ya maji makao makuu ya wilaya yetu, na pale kuna hospitali ya wilaya ambayo pia itapata huduma ya maji. Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa mambo ambayo anawafanyia wana-Rorya. Hakuna kama Mama Samia,” amesema Chikoka.

Amewataka wananchi wa vijiji vitakavyopitiwa na mradi huo kutoa ushirikiano na kuwa walinzi wa miundombinu ya maji, huku akionya kuwa watakaobainika kuhujumu miradi watakuwa ‘wameingia 18 zake’.

DC Chikoka (katikati) akizungumza na wananchi kijijini Raranya mara baada ya kupokea shehena ya bomba hayo

Ofisi ya RUWASA Wilaya ya Rorya imesema mabomba hayo yatasambazwa kwenye eneo lenye urefu wa takriban kilomita 19.

“Leo tumepokea bomba ya inchi 140 yenye urefu wa mita 1,680 na inchi 2.5 yenye urefu wa mita 900. Tulishapokea shehena nyingine na mzigo mwingine upo njiani unakuja,” amesema Mhandisi Moses Magehema wa RUWASA Rorya.

Kwa upande wake, Ofisa Maendeleo ya Jamii wa RUWASA Rorya, Emmanuel Bulugu amesema mradi huo utanufaisha takriban wananchi 24,000 katika vijiji vya Raranya, Bukama, Ingiri Juu, Malongo na Ryagoro.

Mradi huo unatekelezwa katika awamu mbili; ambapo Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) itajenga mtandao wa maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria katika eneo la Shirati na kuyafikisha kijijini Raranya.

RUWASA itaweka miundombounu ya kuyasambaza katika makao makuu ya wilaya na vijiji jirani, kikiwemo Raranya.

Mkuu wa Wialaya, Chikoka, ametaka wananchi wazawa kupewa fursa za ajira wakati wa utekelezaji wa mradi huo, ili uweze kuwa na faida za kiuchumi kwao.

(Habari na Picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages