NEWS

Friday 24 June 2022

Serikali mkoani Mara yautaka umma kupuuza upotoshaji kuhusu ujenzi wa kituo cha afya Makongro wilayani Rorya



SERIKALI mkoani Mara imeutaka umma wa wananchi kupuuza opotoshaji unaoenezwa na watu wachache, kuhusu utaratibu wa kupata eneo la ujenzi wa kituo cha afya Makongro katika kata ya Rabuor wilayani Rorya.

Taarifa kwa umma, iliyotolewa na Ofisi yaa Mkuu wa Mkoa huo jana, imesema uamuzi wa kujenga kituo hicho ulifikiwa na mamlaka husika, kwa kuzingati vigezo na taratibu za kisheria.

Taarifa hiyo imetaja vigezo vilivyozingatiwa kuwa ni pamoja na kupatikana kwa eneo lenye ukubwa wa ekari zaidi ya 10 unotosha majengo 12 yanayohitajika, ambalo limetolewa kwa hiari na wamiliki kwa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.

Pia, imesema eneo hilo limepitishwa na wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) ya Rabuor kupitia vikao halali vya kisheria, lipo katika jiografia rafiki na linafikika kwa urahisi.

“Ujenzi wa kituo umeshanza na umefikia hatua ya lenta. Kituo hiki kikikamilika kitatumiwa na wananchi wa tarafa nzima ya Luo-imbo kama rufaa ya zahanati zilizopo.

“Aidha, katika kijiji jirani cha Oliyo, Serikali Kuu imepeleka shilingi milioni 50 kwa ajili ya kukamilisha zahanati.

“Ndugu wananchi, uongozi wa Mkoa unawaomba kupuuza upotoshaji wowote kuhusu ujenzi wa kituo hiki cha afya. Mkoa utaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuzingatia ubora na thamani ya fedha,” imeeleza sehemu ya taarifa iliyosainiwa na Kaimu Afisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Stephano Amoni.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages