NEWS

Sunday 5 June 2022

Serikali yawapiga msasa walezi wa vituo vya kulea watoto wadogo Tarime-Rorya



WALEZI 59 wa vituo vya kulea watoto wadogo katika Kanda Maalum ya Tarime-Rorya wamepata mafunzo ya wiki mbili kuhusu malezi na makuzi bora ya watoto hao.

Mafunzo hayo yamehitimishwa mjini Tarime juzi na Yohana Ryoba ambaye ni Maratibu wa Programu ya Mafunzo ya Malezi, Makuzi na Malezi ya Awali ya Mtoto - inayoratibiwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, Wanawake na Mkundi Maalumu.


Ryoba amesema mafunzo hayo yametolewa kuwajengea walezi wa vituo hivyo uwezo wa kuelekeza watoto namna makuzi yanavyojengeka katika maisha yao.


“Tumewajengea uwezo wa kuwafundisha watoto kukua vizuri kimaadili, kiakili, kijamii, kihisia na kimwili ili waweze kukua vema na kuwa zao bora la jamii.

“Tumehitimisha mafunzo kwa wahitimu 59 katika Kanda Maalum ya Tarime-Rorya na 150 Musoma ili kuwajengea uwezo wa malezi ya kifamilia kwa sababu wanajamii wanaenda na majukumu yao ya utafutaji mali wanaacha watoto katika vituo hivi, wasipolelewa kwa maadili bora mwisho tutakuwa na ‘panya road’, watoto wa mitaani na wasiokuwa na makuzi bora.

“Kwa hiyo, Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeona ni vema kuwajengea uwezo hawa walezi waweze kutoa mafunzo bora kwa mustakabali bora wa taifa lililo bora,” amesema Mratibu huyo.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages