NEWS

Sunday 5 June 2022

Waziri Chana asitisha usafirishaji wanyamapori hai nje ya Tanzania



WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt Pindi Chana (pichani), leo amesitisha hatua ya kusafirisha wanyamapori hai nje ya nchi, iliyotangazwa jana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamnapori Tanzania (TAWA).

“Kama waziri mwenye dhamana ya masuala yote ya maliasili na utalii, nachukua nafasi hii kusitisha mara moja usafirishaji wa wanyamapori hao, mpaka hapo Serikali itakapopata taarifa rasmi kutoka katika taasisi husika.

“Na naomba tuelewane, zoezi hilo la usafirishaji wa wanyamapori limesitishwa mara moja hadi hapo Serikali itakapopata taarifa rasmi kutoka katika taasisi husika na Serikali kuamua vinginevyo.

“Hivyo kwa maelezo yangu haya, hakuna tena usafirishaji wa wanyamapori hao kama jinsi ambavyo tangazo hilo la jana limetolewa na hiyo taasisi,” amesisitiza Waziri Chana.

Tangazo kwa umma lililotolewa na Kamishna wa Uhifadhi TAWA, lilisema Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ilifanya tathmini ya biashara ya usafirishaji wanyamapori hai nje ya nchi baada ya kuweka zuio la biashara hiyo mwaka 2016.

“Kufuatia tathmini hiyo, Serikali imeruhusu usafirishaji wa wanyamapori waliokuwa wamesalia kwenye mazizi na mashamba ya ufugaji baada ya zuio,” ilieleza sehemu ya tangazo hilo na kufafanua kuwa ruhusa hiyo ni ya kipindi cha miezi sita kuanzia Juni 6 hadi Desemba 5, 2022.

Tangazo lilieleza kuwa ili kufanikisha shughuli hiyo, wafanyabiashara wenye wanyamapori waliosalia kutokana na biashara ya wanyamapori hai na ambao wamefanyiwa uhakiki wanatakiwa kuwasilisha nyaraka zote muhimu katika Ofisi za Utalii na Huduma za Biashara zilizopo jijini Arusha na Dar es Salaam.

“Usafirishwaji wa wanyamapori hao utafanyika kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

“Wadau watakaoruhusiwa kusafirisha wanyamapori ni wale wenye leseni ya Biashara ya Nyara (TDL) zilizohuishwa kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009,” lilisisitiza tangazo hilo la TAWA.

#MaraOnlineNews-Updates

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages