NEWS

Friday 10 June 2022

Shirika la Maji Safi Group lakutanisha wanafunzi, walimu, wazazi na viongozi wa dini wilayani Butiama kujadili makuzi na hedhi salama kwa watoto



SHIRIKA la Maji Safi Group limekutanisha wanafunzi, wazazi, walimu na viongozi wa dini wilayani Butiama, kujadili makuzi na hedhi salama kwa watoto, ambapo mabinti wametumia fursa hiyo kuomba huduma ya taulo za kike ipatikane hadi kwenye maeneo ya kuabudia.

“Tunaomba madhehebu ya dini nayo yawe na huduma ya pedi [taulo za kike] ili kusaidia wanaoingia hedhi wakiwa maeneo ya ibada,” amesema mmoja wa wanafunzi wa kike walioshiriki mkutano huo katika Shule ya Sekondari ya Kukirango, Juni 8, 2022.


Aidha, mwanafunzi huyo (jina limehifadhiwa) amesema elimu ya hedhi salama na upatikanaji wa taulo za kike, maji safi na vyumba vya kujisitiri vizingatiwe, hususan katika shule zote za sekondari, ili kuwezesha watoto wa kike kusoma kwa amani hata wanapokuwa kwenye hedhi.

Walimu, wazazi na viongozi wa dini wameahidi kuunga mkono Shirika la Maji Safi Group katika kueneza elimu ya hedhi salama kwa watoto, huku wakiwataka mabinti kutoonea aibu suala la hedhi.


“Watoto wa kike wavunje ukimya, wasionee aibu suala la hedhi, na sisi viongozi wa dini tuko tayari kuliandalia shirika hili [Maji Safi Group] mazingira ya kuleta elimu hii kwa waumini wa madhehebu yetu,” amesema Katibu wa BAKWATA Wilaya ya Butiama, Dkt Mohamed Nyongoti.

Dkt Nyongoti (aliyesimama kulia) akizungumza katika mkutano huo

Kuhusu mimba na ndoa za utotoni, wanafunzi wa kike wamehimizwa kuepuka ngono na vitendo vingine vinavyoweza kuwaingiza katika matatizo hayo na hatimaye kuua ndoto zao za kielimu.

“Wanafunzi wa kike mnapaswa kujitambua na kujiamini, someni kwa bidii na kujihadhari dhidi ya mimba na ndoa za utotoni ili muweze kufikia dira za maisha yenu baada ya masomo,” amesisitiza Mratibu wa SWASH Mkoa wa Mara, Mwalimu Judith Mrimi.
Mwalimu Judith (katikati) akizungumza mkutanoni

Naye mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Kukirango, Lameck Nicholaus, amewahimiza watoto wa kike kuishi kwa maadili, kusoma kwa bidii, kuheshimu wazazi, walimu na sheria za shule, ili waweze kufikia malengo yao kielimu.

Awali, Mkurugenzi wa Shughuli za Utekelezaji kutoka Shirika la Maji Safi Group lililopo Rorya mkoani Mara, Rachel Stephen amesema waliamua kukutanisha makundi hayo ya jamii ili kutengeneza jukwaa la kujadili kwa pamoja suala la makuzi na hedhi salama kwa watoto.

Rachel (kushoto) akielezea umuhimu wa mkutano huo

Rachel amefafanuwa kuwa katika shule za sekondari walizopita wilayani Butiama kutoa elimu ya makuzi na hedhi salama kwa watoto, walibaini kwamba wanafunzi wengi wanahitaji kukutanishwa na wazazi wao kueleza changamoto zao.


“Tumekuwa tukijikita kufundisha mashuleni huku Butiama, lakini changamoto kubwa inaonesha watoto wanatamani tuwaweke pamoja na wazazi wao waongee, ili zile changamoto ambazo labda wanashindwa kuongea wakiwa nyumbani waweze kuziongea mbele ya wazazi,” amesema Rachel na kuendelea:

“Kupitia mkutano au jukwaa hili, wazazi, walezi, walimu na viongozi wa dini wanabadilishana uzoefu wao, watoto nao wanabadilishana uzoefu na kueleza changamoto wanazokutana nazo katika suala zima la makuzi na hedhi salama.”


Mkurugenzi Rachel amesema lengo kuu ni kuwezesha makundi hayo ya jamii kupata uelewa wa pamoja, ili hatimaye yaweze kuzungumza na kutatua changamoto za hedhi na makuzi zinazowakabili watoto, hasa wa kike, ambazo zinawasababisha kukosa masomo kwa baadhi ya siku.

“Mkutano huu umekuwa na mafanikio kwa sababu watoto wametumia nyimbo na mashairi, wamesimama na kuongea changamoto wanazokutana nazo, lakini pia wameeleza mambo ambayo wanadhani jamii; wazazi, walimu na viongozi wa dini wanapaswa kufanya ili kutatua changamoto zao,” amesema Rachel.


(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages