WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Tarime mkoani Mara, imezitunuku shule mbili na taasisi mbili vyeti vya pongezi kutokana na juhudi kubwa zilizoonesha katika uhifadhi wa mazingira, kwa kupanda na kutunza vizuri miche ya miti.
Shule za aekondari zilizotunukiwa vyeti hivyo ni Kewamamba na Nyansisime na taasisi ni Kituo cha Masista Kitenga na 822KJ Kiteule cha Tarime, ambazo zimeonesha ufanisi katika kupanda na kutunza miche ya miti ya aina mbalimbali iliyotolewa na TFS hiyo.
Mhifadhi Massawe na Sista wa Kitenga wakionesha cheti cha pongezi
Awali, akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vyeti hivyo iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Kewamamba leo Juni 7, 2022, Mhifadhi Misitu wa Wilaya ya Tarime, Charles Massawe amesema usambazaji wa miche ya miti kwenye taasisi mbalimbali ni moja ya majukumu ya TFS.
Mhifadhi Massawe amesema katika mwaka wa fedha 2021/2022, ofisi yake ilipanga kusambaza miche ya miti 75,000 lakini imefanikiwa kuvuka lengo kwa kusambaza miche 83,140 sawa na asilimia 111, kwa taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi wilayani Tarime.
Ametaja taasisi zilizosambaziwa miche hiyo kuwa ni pamoja na shule za msingi na sekondari, vituo vya afya, dini na majeshi ya ulinzi na usalama.
“Miche [83,140] tuliyosambaza inatosha kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 187,” amesema Massawe.
Mhifadhi Misitu huyo amesema ufuatiliaji uliofanywa na ofisi yake umebaini kuwa asilimia 70 ya miche hiyo waliyosambaza inaendelea kukua vizuri.
Hata hivyo, Massawe amesema katika baadhi ya maeneo miche iliyopandwa ilikumbwa na vikwazo mbalimbali, ikiwemo kuharibiwa na mifugo, kuibwa, kuathiriwa na maji mengi na kuliwa na mchwa.
“Kutokana na hali hiyo, TFS Wilaya ya Tarime tumeshauri taasisi husika kuendelea kushirikiana na viongozi wa vijiji na mitaa katika kuelimisha wananchi umuhimu wa kutunza mazingira kwa kupanda na kutunza miti kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla,” amesema Mhifadhi Massawe.
Akikabidhi vyeti vya pongezi kwa uongozi wa shule za sekondari Kewamamba na Nyansisime, Kituo cha Masista Kitenga na 822KJ Kiteule cha Tarime, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Col Michael Mntenjele ametoa wito kwa wananchi kutambua kuwa kila mmoja ana jukumu la kupanda miti na kutunza mazingira kwa maendeleo endelevu.
Col Mntenjele (kushoto) akimkabidhi Afisa wa 822KJ Kiteule cha Tarime cheti cha pongezi. |
“Kwa hiyo, tusiharibu mazingira, tulinde ikolojia ya Bonde la Ziwa Victoria, ukiwemo Mto Mara wenye mchango katika uhifadhi wa wanyamapori, wakiwemo nyumbu ambao huuvuka kila mwaka ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti,” amesema Col Mntenjele na kutoa wito kwa kila kaya kupanda miti ya matunda isiyopungua miwili kwa ajili ya lishe bora na kutunza mazingira.
Col Mntenjele (kushoto) akimkabidhi Mwalimu John Sausi cheti cha pongezi
Mipango ya TFS Wilaya ya Tarime kwa mwaka wa fedha 2022/2023, kwa mujibu wa Massawe, ni pamoja na kusambaza miche ya miti laki moja, ambapo nguvu kubwa itaelekezwa kwa watu binafsi.
Hafla ya kukabidhi vyeti hivyo imehudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Daniel Komote na Mkuu wa Shule ya Sekondari Kewamamba, Mwalimu John Sausi, miongoni mwa viongozi wengine wa taasisi za umma, zikiwemo za majeshi ya ulinzi na usalama.
(Habari na picha zote: Mara Online News)
No comments:
Post a Comment