NEWS

Thursday 4 August 2022

DAS Tarime akiri kupata taarifa za tukio la RMO Mara kumshambulia mtumishi wa kike usiku




Na Mara Online News
---------------------------

KATIBU Tawala wa Wilaya (DAS) ya Tarime, John Marwa amekiri kupata taarifa za tukio la Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO) wa Mara, Dkt Juma Mfanga kumshambulia mtumishi wa kike usiku katika Hospitali ya Nyamwaga.

“Jambo hilo lipo, labda Mkurugenzi anaweza kueleza vizuri limefikia wapi, lakini taarifa nilizipata,” DAS Marwa ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu leo mchana.

DAS huyo amekataa kuzungumzia zaidi suala hilo akisema siyo msemaji.

Taarifa za tukio hilo ziliripotiwa katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari kutoka serikalini.

Jana, Mara Online News iliandika habari za tukio hilo zinazoeleza kuwa siku chache zilizopita, Dkt Mfanga alifika katika Hospitali ya Nyamwaga usiku na kuzusha mvutano mkubwa wa mazungumzo na mmoja wa watumishi wa hospitali hiyo.

Inaelezwa kuwa wakati wa mvutano huo, RMO huyo alimshambulia kwa kumsukuma mtumishi huyo (jina lipo) hadi akaanguka na kuumia sehemu ya kichwa.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, baada ya shambulio hilo mtumishi huyo alisindikizwa na wenzake kwenda kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Nyamwaga ili kupata PF3 kwa ajili ya matibabu.

Taarifa zaidi zinaelezwa kuwa Dkt Mfanga alimuomba msamaha mtumishi huyo akakubali kumsamehe na hivyo suala hilo likaishia hapo kabla ya kuingizwa kwenye kitabu cha malalamiko.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa baada ya maafikiano hayo, RMO huyo baadaye aliwafuata baadhi ya watumishi wa hospitali hiyo na kutoa vitisho, vikiwemo vya kusudio la kuwahamishia nje ya mkoa wa Mara.

Inadaiwa kuwa Dkt Mfanga amekuwa akilindwa na mmoja vigogo wizarani na kwa muda mrefu sasa, amekuwa akinyanyasa watumishi wa afya katika halmashauri za mkoa wa Mara na kuwavunja moyo wa kuhudumia wagonjwa.

“Kwa mfano kuna mtumishi wa kituo cha afya Magoma wilayani Tarime ambaye amelazimika kuacha kazi kutokana na maneno ya kuudhi yakiwemo matusi ya nguoni na vitisho kutoka RMO huyo.

“Sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma ziko wazi kuhusu namna ya kumwajibisha mtumishi anapoonekana kufanya kosa, lakini huyo RMO amekuwa akienda kinyume na miongozo hiyo ya Serikali,” kimedokeza chanzo chetu cha habari kwa sharti la kutotajwa jina.

Baada ya taarifa za tukio hilo kuripotiwa na Mara Online News tangu jana, watumishi wa afya kutoka hospitali mbalimbali za mkoani Mara wamepiga simu kwenye chumba cha habari na kufunguka jinsi wanavyonyanyaswa na Dkt Mfanga.

Wataalamu wa afya wa Serikali wanasema vitendo vya unyanyasaji vikiwemo vya matusi vinavyofanywa na RMO huyo ni hatari kwa utoaji wa huduma bora za matibu katika mkoa wa Mara.

“Ameumiza watu wengi kimwili na kisaikolojia, siyo Tarime tu, hata Musoma Vijijini mpaka ofisini kwake kuna watumishi wanalalamika kunyanyaswana na RMO huyo.

“Mtumishi wa afya akishakuwa disturbed anakosa molari ya kuhudumia wagonjwa. Hii ni hatari sana, mamlaka za uteuzi zitazame upya vigezo vya kuwapa watu madaraka ya RMO.

“Kosa la kufanya shambulio la mwili kwa mtumishi mwenzake ni kati ya makosa makubwa yanayoweza kumfukuzisha kazi.

“Hakuna mahali RMO anaruhusiwa kufanya kazi usiku bila kumtaarifu Mkurugenzi na Mganga Mkuu wa wilaya husika, shambulio alilofanya ni kosa la jinai,” amesema mmoja wa madaktari wa Serikali mkoani Mara.

Alipoulizwa na Mara Online News kwa njia ya simu jana saa tano asubuhi, Dkt Mfanga alidai kuwa alikuwa kikaoni na kuahidi kupiga simu baada ya kikao.

Hata hivyo, baada ya Mara Online News kusubiri hadi saa 10 jioni iliamua kumpigia Dkt Mfanga simu tena ambapo iliita bila kupokewa.

Hivyo, Mara Online News iliamua kumtumia ujumbe mfupi wa maneno (sms), ndipo baadaye akajibu kwa kifupi “Fika ofisini… huyo aliyekutuma mwambie akuwezeshe na nauli”.

Bado Mara Online News inaendelea na juhudi za kuwapata Mawaziri wenye dhamana; Ummy Mwalimu wa Afya na Innocent Bashungwa wa TAMISEMI, kwa ajili ya kuzungumzia suala la tuhuma hizo zinazoelekezwa kwa RMO huyo.

Jumatatu iliyopita, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza katika hafla ya kuapisha Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa wapya, aliwasisitiza viongozi wote wa umma kusimamia sheria, kanuni na taratibu na kuhakikisha haki inatendeka kwa watumishi na wananchi kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages