NEWS

Monday 5 September 2022

Barrick North Mara yazindua mashindano ya Mahusiano Cup
Na Mwandishi Wetu, Nyamongo
-------------------------------------------

KAMPUNI ya Barrick North Mara imezindua mashindano ya soka ya Kombe la Mahusiano “Mahusiano Cup”, mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele ambaye amekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo.

Uzinduzi huo ulifanyika jana kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Ingwe mjini Nyamongo, ambapo mashindano hayo ya siku 15 [Septemba 4 hadi 18, mwaka huu] yatashirikisha vijiji 16.

Kanali Mntenjele (mwenye kofia) na Mbunge Waitara wakikagua timu wakati wa uzinduzi huo

Vijiji hivyo vinavyoshiriki mashindano hayo ni Genkuru, Msege, Komarera, Nyamwaga, Kewanja, Nyakunguru, Kerende, Nyabichune, Mjini Kati, Matongo, Nyangoto, Mrito, Keisangora na Nyarwana.

Mashindano hayo yameandaliwa na Kampuni ya Barrick North Mara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, yakiwa na kaulimbiu inayosema “Mahusiano Bora kwa Uwekezaji Endelevu.”


Kampuni ya Barrick ilisema itatumia mashindano hayo kukuza na kudumisha mahusiano mema kati ya Mgodi wa Dhahabu wa North Mara na jamii inayouzunguka.

Aidha, mashindano hayo yatasaidia kuongeza uelewa juu ya fursa mbalimbali zilizopo na kushughulikia masuala mtambuka, hasa uvamizi, uharibifu wa miundombinu (vandalism) na utegeshaji wa mazao, miti na nyumba.

Awali, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko alisema michezo ni nyenzo muhimu ya katika kujenga na kudumisha mahusiano.

“Bila mahusiano bora sisi kama kampuni hatuwezi kufanya kazi kwa utulivu na jamii inayotuzunguka haiwezi kupata manufaa,” alisema Meneja Lyambiko.


Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo

Mkuu wa Wilaya, Kanali Mntenjele aliwataka washiriki wa mashindano hayo kucheza kwa amani na wasimamizi husika kutenda haki bila kupendelea timu yoyote.

Naye Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara aliipongeza Barrick North Mara kwa kuandaa mashindano hayo, akisema yatahamasisha ushirikiano kutoka kwa jamii inayozunguka mgodi huo ili kuwezesha kila upande kunufaika.

Mbunge Waitara akishiriki kucheza ngoma ya asili wakati wa uzinduzi huo

Uzinduzi wa mashindano ya soka ya Mahusiano Cup pia ulitanguliwa na michezo mbalimbali ikiwemo ya kuvuta kamba, kufukuza kuku na ngoma ya asili, kabla ya timu za Kewanja FC na Mosege FC kucheza mechi ya ufunguzi.Chanzo: Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages