NEWS

Friday, 9 May 2025

Serikali yataja vipaumbele utekelezaji miradi ya Gridi ya Taifa ya Maji, Waziri Aweso aanika mafanikio bungeni



Waziri wa Maji, Jumaa Aweso , akionesha mkoba wenye majabrasha ya makadirio ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2025/2026 alipowasili bungeni jijini Dodoma jana.
----------------------------------------

NA MWANDISHI WETU, Dodoma

SERIKALI imesema imeelekeza nguvu zake katika utekelezaji wa miradi ya Gridi ya Taifa ya Maji inayolenga kutumia vyanzo vikubwa vya maji kama vile mito na maziwa, ili kukidhi mahitaji ya sehemu zinazokabiliwa na uhaba wa rasilimali hiyo nchini.

Gridi ya Taifa ya Maji ni mfumo wa kitaifa wa usambazaji maji safi na salama kutoka maziwa na mito kwa ajili ya kuwafikia wananchi wengi, viwanda na maeneo mengine ya kiuchumi yenye uhaba wa maji.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, aliliambia Bunge jijini Dodoma jana kwamba azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha kwamba huduma ya maji inawafikia wananchi wengi zaidi vijijini na mijini.

Waziri Aweso aliyasema hayo wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka fedha 2025/2026, ambapo aliomba Bunge liidhinishe shilingi 1,016,894,958,000 kwa ajili ya matumizi ya wizara hiyo.

Alisema Wizara ya Maji imeweka vipaumbele vya sekta ya maji ambavyo ni pamoja na kutekeleza miradi ya Gridi ya Taifa ya Maji, ukiwemo mradi kabambe wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda miji ya Dodoma na Singida.

Mradi mwingine wa Gridi ya Taifa ni kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa, mradi wa kutoa maji kutoka Mto Ruvuma kwenda mikoa ya jirani ya Lindi na Mtwara, na mradi wa kutoa maji kutoka Mto Rufiji kwenda mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Pia, ipo miradi kadhaa itakayotekelezwa ya kutoa maji kutoka maziwa ya Victoria na Nyasa ili kufikia vijiji jirani na vyanzo hivyo vya maji, kwa mujibu wa Wizairi Aweso.

Waziri huyo alitaja vipaumbele vingine vya sekta ya maji kuwa ni kutekeleza miradi ya maji 1,539 inayoendelea, ambapo miradi 1,313 inatekelezwa vijijini na 226 mijini, ikiwemo miradi mikubwa ya kimkakati katika maeneo mbalimbli nchini.

Aweso aliongeza kuwa vipaumble vingine vya sekta ya maji ni kukamilisha Mpango Kabambe wa Taifa wa Maji, kuimarisha uhifadhi na utunzaji wa vyanzo vya maji na uendelezaji wake, hasa uchimbaji wa visima na ujenzi wa miundombinu ya uvunaji wa raslimali hiyo.

Vipaumbele vingine ni uimarishaji na udhibiti wa ubora wa maji kwa kuhakikisha yanakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa na kuimarisha utoaji wa huduma kuzuia upotevu wa maji.

Katika kuwasilisha bajeti ya wizara yake, Waziri Aweso aliyataja mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne (2021-2025) ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yenye kuonesha kuimarika kwa sekta ya maji nchini.

Mafanikio hayo ni pamoja na kukamilika na kuridhiwa kwa Sera ya Taifa ya Maji ya Mwaka 2002, Toleo la 2025. Sera hiyo inailekeza wizara kuratibu na kuwa na mipango ya pamoja na sekta nyingine zinazotekeleza miradi inayohusu maji, ikiwemo sekta binafsi.

Mafanikio mengine, kwa mujibu wa Aweso, ni kukamilika kwa miradi ya maji 2,612 vijijini na mijini na kuboreshwa kwa upatikanaji wa maji vjijini kwa asilimia 70.1 mwaka 2020 hadi asilimia 83 Desemba 2024, na kwa maeneo ya mijini kutoka asilimia 84 hadi asilimia 91.6.

Waziri aliliambia Bunge kwamba baadhi ya miradi iliyokamilika ni awamu ya kwanza ya mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda miji ya Tinde na Shelui, mradi wa ujenzi wa mfumo wa kutibu maji katika mji wa Bunda, ujenzi wa chanzo cha maji Butimba, mradi wa Kyaka/Bunazi mkoani Kagera, mradi wa Orkesumet, mradi wa Dareda, Singu, Sigino mkoani Manyara na miradi 218 chini ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19.

Hali kadhalika, ipo miradi iliyokwamuliwa baada ya utekelezaji kukaa muda mrefu bila kuendelezwa. Miradi hiyo ni Same - Mwanga - Korogwe, Bunda – Mugango -Kiabakari - Butiama na ujenzi wa tekeo la maji katika mji wa Kigoma, kwa kutaja miradi michache.

Waziri Aweso pia alisema wizara yake inajivunia kuanza kwa utekelezaji wa miradi ya kimkakati, ukiwemo mradi wa miji 28 nchini.

Jukumu la msingi la Wizara ya Maji ni kutayarisha na kusimamia utekelezaji wa sera, mikakati na programu ya maendeleo ya sekta ya maji kwa ujumla.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages