NEWS

Monday 5 September 2022

Begha alivyoifuta CHADEMA Serengeti



Jacob Begha

Na Mwandishi Wetu, Serengeti
-----------------------------------------

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Serengeti, Jacob Begha ametaja mafanikio makubwa anayojivunia katika uongozi wake kuwa ni pamoja na ‘kufuta ngome’ ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani hapa.

“Kipindi nachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Serengeti, mimi na viongozi wengine wa chama wilayani hapa tulikua kama yatima, maana hatukuwa na Mbunge wala Mwenyekiti wa Halmashauri aliyetokana na Chama Cha Mapinduzi. Unaweza ukaona ugumu uliokuwepo katika kuanza kukijenga chama na kukirejesha kwenye makali yake.

“Kipindi hicho, yaani mwaka 2017, Jimbo la Serengeti lilikuwa chini ya Mbunge kutoka CHADEMA na Halmashauri ya Wilaya yetu ilikuwa inaongozwa na Mwenyekiti kutoka CHADEMA pia,” alisema Begha katika mahojiano na Sauti ya Mara mjini Mugumu, juzi.

Hata hivyo, Begha alisema mwaka 2018 aliweza kushirikiana na viongozi wenzake kushawishi Mbunge Marwa Ryoba na Mwenyekiti wa Halmashauri, Juma Porini wakahamia CCM pamoja na madiwani wanane kutoka CHADEMA.

“Kitendo cha Mbunge, Mwenyekiti wa Halmashauri na madiwani wanane kuhamia Chama Cha Mapinduzi kilitoa nafasi ya Jimbo na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuwa chini ya uongozi wa chama chetu [CCM],” alisema Begha.

Aidha, katika uchaguzi wa wenyeviti wa vitongoji na vijiji mwaka 2019, CCM chini ya uongozi wa Begha kama Mwenyekiti wa Wilaya, kilifanikiwa kurejesha vitongoji na vijiji vyote kwenye himaya yake.

“Pia katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020, CCM chini ya uongozi wangu kama Mwenyekiti wa Wilaya, kilifanikiwa kushinda kiti cha ubunge na viti vya udiwani katika kata zote 30 wilayani Serengeti,” aliongeza Mwenyekiti Begha ambaye mwaka huu anatetea nafasi hiyo.

Matarajio yake
Begha alisema matarajio yake ikiwa atachaguliwa tena ni kuendelea kuimarisha CCM katika nyanja zote ili kiendelea kushika Dola nchini.

“Vile vile nitaendelea kusimamia Ilani ya CCM kwani Mwenyekiti wetu Mahiri na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameonesha kuisimamia na kuitekeleza kwa vitendo.

“Tumeshuhudia ujenzi wa vyumba vya madarasa 119 kwa mkupuo wilayani Serengeti na mradi wa maji wa bwawa letu la Manchira ambao ulikuwa kizungumkuti kwa muda mrefu.

“Lakini pia ujenzi wa vituo vya afya vitatu vinavyojengwa kwa kasi na muda mchache vitaanza kazi, ujenzi wa high schools na miradi mingi ya kijamii,” Alisema Begha na kuongeza:

“Si hivyo tu, Filamu ya Loyal Tour ambayo imefungua utalii katika wilaya yetu ni jambo ambalo linapaisha uchumi wetu wa Serengeti. Kadhalika mikopo ya riba nafuu ya asilimia 10 kwa vikundi mbalimbali, lakini pia mikopo isiyo na riba kwa wafugaji nchini.”

Pamoja na mipango mingi iliyopo, Mwenyekiti Begha alitaja mambo mawili makubwa ni kuwa kujenga uzio katika Uwanja wa Mpira Sokoine ambao ni chanzo cha mapato cha CCM Wilaya ya Serengeti.

“Jambo la pili ni ujenzi wa ofisi ya CCM Wilaya ya Serengeti, ramani zipo tayari na mipango ya awali ilikwishaanza kupitia Kamati iliyoundwa na wawekezaji ambao baada ya corona kazi itaendelea kuratibiwa kichama na tayari walikwishaelekeza akaunti kwa michango ya ujenzi,” aliongeza Begha.

Chanzo: Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages