NEWS

Wednesday 14 September 2022

Makamu wa Rais Dkt Mpango aiagiza MWAUWASA kuwapa kipaumbele wananchi wanaoishi jirani na dakio la maji Butimba
Na Mara Online News
-----------------------------

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Philip Mpango (wa pili kushoto pichni juu), ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kuwapa wananchi wanaoishi jirani na dakio la maji Butimba kipaumbele katika kupata huduma hiyo.

Dkt Mpango ametoa maelekezo hayo leo Septemba 14, 2022 wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa dakio jipya la maji katika eneo la Butimba jijini Mwanza.

Aidha, amemtaka mkandarasi kuharakisha ujenzi wa mradi huo - akisema ukikamilika kuelekea Sikukuu ya Krismasi mwaka huu utakuwa zawadi kwa wakazi wa jiji la Mwanza.

Sambamba na hilo, Makamu wa Rais ameilekeza MWAUWASA kuhakikisha muda wa kuunganishia wateja huduma ya maji haizidi siku saba.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, Serikali imedhamiria kuondolea wakazi wa jiji la Mwanza tatizo la uhaba wa maji kwa kujenga miradi mikubwa ya huduma ya majisafi ya bomba kutoka Ziwa Victoria.

“Serikali inatambua kasi ya ukuaji wa jiji la Mwanza pamoja na changamoto ya upatikanaji wa majisafi katika baadhi ya maeneo ya pembezoni na yale yenye miinuko mikali, mradi huu kwa kiasi kikubwa utaboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwenye maeneo mengi,” amesema Dkt Mpango.

Amebainisha kuwa mradi huo utagharimu shilingi bilioni 69 na utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia wakazi zaidi ya 450,000.

Makamu wa Rais Dkt Mpango ameyataja maeneo yakayaonufaika na mradi huo kuwa ni pamoja na Nyegezi, Mkolani, Buhongwa, Lwanhima, Fumagila, Sahwa, Igoma, Kishiri na Nyamhongolo.

Pia maeneo ya Usagara, Nyashishi na Fella katika wilaya ya Misungwi, Kisesa, Bujora na Isangijo wilayani Magu yatanufaika na mradi huo.

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea na jitihada za dhati za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini ili kuhakikisha huduma za msingi za kijamii zinapatikana kwa wananchi wote,” amesema Dkt Mpango.

Awali, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akizungumza amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025, upatikanaji wa huduma ya maji kwa maeneo ya mijini unafika asilimia 95 na vijijini asilimia 85.

Waziri Aweso amesema pamoja na mradi huo kuwa na uwezo wa kuzalisha lita za ujazo milioni 48 kwa siku, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa kimaendeleo itaendelea na ujenzi wa awamu ya pili ya mradi huo na uboreshaji wa chanzo cha maji cha Capri Point ili kutosheleza mahitaji ya wakazi wa jiji la Mwanza ambalo kwa sasa linahitaji lita milioni 160 kwa siku.

“Natambua kazi kubwa inayofanywa na Mamlaka ya Majisafi Mwanza [MWAUWASA], wanapambana usiku na mchana katika kuhakikisha huduma ya maji inakuwa nzuri,” amesema.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages