NEWS

Monday 12 September 2022

Professor Mwera Foundation yang’ara Maadhimisho Juma la Elimu ya Watu Wazima
Na Mwandishi Wetu, Tarime
-------------------------------------
TAASISI ya Professor Mwera Foundation (PMF) imepongezwa kwa ushiriki mzuri katika Madhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima (EWW) wilayani Tarime, Mara.

Pongezi hizo zilitolewa na Mwakilishi wa Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Martha Omahe aliyekuwa mgeni rasmi katika uhitimishaji wa maonesho hayo kwenye viwanja vya Chuo cha Ualimu Tarime, Ijumaa iliyopita.

“Nimeona shughuli zenu ni nzuri, zinasaidia jamii - ikiwemo kuwezesha vijana kupata mafunzo ya fani mbalimbali na stadi za ujasiriamali,” alisema Omahe ambaye ni Afisa Tarafa ya Inano.

Omahe alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito wa kuhamasisha wazazi na walezi kupeleka watoto wao kusoma katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi na Shule ya Sekondri ya Wasichana Tarime vimavyomilikiwa na Taasisi ya PMF.

Kwa upande wake, Meneja Uendeshaji wa PMF, Mwalimu Mwita Samson Marwa alieleza kufurahishwa na namna watu mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa shule za sekondari na chuo cha ualimu walivyovutiwa na shughuli zinazoendeshwa na taasisi hiyo.“Watu wamepata fursa ya kuona na kujua shughuli zetu kama vile mafunzo ya kompyuta, udereva, ufundi umeme, magari, ushonaji, usimamizi wa maabara, hoteli na uongozaji watalii,” alisema Mwalimu Mwita.

Naye Mkuu wa Chuo cha Mgunzo ya Ufundi Tarime, Mwalimu Frank Joashi alishauri Halmashauri za Mji na Wilaya ya Tarime kuongeza juhudi za hamasa ili wadau wengi waweze kuhudhuria maonesho ya EWW yajayo.

Taasisi ya Professor Mwera Foundation yapo mjini Tarime yenye makao makuu mjini Tarime, iliasisiwa na Peter Mwera na inaendeshwa chini ya Mkurugenzi wake, Hezbon Peter Mwera ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Kanda ya Ziwa.

Majukumu mengine
Taasisi hiyo imeidhinishwa na Serikali kuendesha programu ya mafunzo ya kitaaluma kwa wafanyakazi wa sekta za hoteli na utalii katika mikoa 10; ambayo ni Mara, Mwanza, Shinyanga, Kagera, Geita, Simiyu, Kigoma, Katavi, Rukwa na Ruvuma.

“Vijana waliopata daraja la nne na alama sifuri wana fursa ya kujiunga na vyuo vya ufundi ili wasijione wametengwa… kupitia vyuo vya ufundi wanaweza kupanda hadi chuo kikuu na hatimaye kuajiriwa, au kujiajiri kutokana na fani walizosoma,” anasema Hezbon.

“Tunahamasisha vijana baada ya kumaliza kidato cha nne wakati wanasubiri matokeo ni vizuri wakajiunga na vyuo vya ufundi wakapata zile fani, matokeo yakitoka yakiwa mazuri, kijana akienda Advance (kidato cha tano) akiwa na fani yake kuna sehemu itamsaidia.

“Lakini matokeo yasipokuwa mazuri, ile fani pia anaweza akajiendeleza nayo na baadaye ikamsaidia kujiajiri au kuajiriwa. Kwa hiyo tuhamasishe vijana kuona umuhimu wa kujiunga na hivi vyuo vya ufundi ambavyo kwa sasa vimeunganishwa na NACTE ili kuviboresha kitaaluma,” anaongeza Mkurugenzi huyo.

Hezbon anampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ya kuiletea nchi maendeleo ya kisekta, ikiwemo kutoa fursa kwa watoto wa kike kuendelea na masomo baada ya kuwa wamekatishwa kwa kupata ujauzito na kujifungua.

Anasema Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime ni moja ya vyuo vikubwa Kanda ya Ziwa, na tayari kimeanzisha mpango wa kusaidia vijana kusoma bure na kwamba hadi sasa kimeshasaidia vijana zaidi ya 3,000.

“Ninamshukuru na kumpongeza Mama [Rais Samia] kwa kufungua mipaka na kuleta fursa nyingi kwa Tanzania, lakini pia kwa maono makubwa ya kuondoa ujinga, umaskini na maradhi. Tunaona juhudi zake katika shule - ametoa fedha za kujenza madarasa ili kuongeza fursa kwa watoto wengi kupata elimu,” anasema Hezbon.

Anaongeza kuwa Rais Samia pia anastahili pongezi kwa kuonesha dhamira ya kuanzisha vyuo vya ufundi kila wilaya nchini.

“Vyuo hivi vitasaidia vijana wengi waliohitimu kidato cha nne, kukata tamaa na kuzurura mitaani kutokana na kukosa ajira,” anasema Mkurugenzi Hezbon.

Chanzo: Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages