NEWS

Monday 19 September 2022

Wananchi watakiwa kulinda Mgodi wa Barrick North Mara


Meneja Mkuu wa Mgodi wa North Mara, Apolinary Lyambiko (aliyesimama) akizungumza katika fainali ya mashindano ya Kombe la Mahusiano, jana. Kushoto kwake ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, John Marwa, miongoni mwa viongozi wengine.

Na Mwandishi Wetu, Nyamongo
------------------------------------------

SERIKALI wilayani Tarime imeeleza kufurahishwa na juhudi zinazofanywa na Kampuni ya Barrick katika kuimrisha mahusiano yake na vijiji vinavyozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kupitia Mashindano ya Soka ya Kombe la Mahusiano.

Akizungumza katika fainali ya mashindano hayo maarufu kwa jina la “Mahusiano Cup” katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Ingwe jana Septemba 18, 2022, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, John Marwa alisema Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa manufaa ya wananchi na mgodi huo.

Marwa alitumia nafasi hiyo pia kuwataka wananchi hao kulinda kwa kupiga vita vitendo vya tegesha, uvamizi na uharibifu wa miondombinu katika mgodi huo.

“Nina imani sasa tutaendelea kulinda mgodi wa North Mara ili tuendelee kunufaika zaidi, na hatutasikia tena vitendo vya tegesha na uvamizi,” alisema Marwa katika hafla ya fainali hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwemo wenyeviti wa vijjiji, madiwani na mamia ya wananchi kutoka vijiji vinavyozungika mgodi huo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, John Marwa akizungumza katika hafla ya fainali hiyo.

Marwa ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Tarime katika hafla hiyo, alishauri uongozi wa mgodi huo kuangalia uwezekano wa kupanua wigo wa mashindano hayo kwa kuhusisha kata zote za wilaya hiyo.

“Ningefurahi zaidi kama mashindano haya yangehusisha wilaya yote ya Tarime,” alisisitiza Marwa.

Mashindano hayo ambayo yamefanyika kwa wiki mbili - yakihusisha timu 16 kutoka vijiji mbalimbali, yalizinduliwa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele, Septemba 4, mwaka huu.
Aidha, Marwa alieleza kufurashwa na kaulimbiu ya mashindano hayo kwa mwaka huu ambayo inasema “Mahusiano Bora kwa Uwekezaji Endelevu”.

“Hatuna budi kuendelea kushirikiana na kudumisha mahusnao kwa sababu mgodi huo unatusaidia kwa namna mbalimbali,” alisema.

Awali, Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko alisema mgodi huo uliandaa zawadi mbalimbali zikiwemo fedha taslimu, medali na mipira kama motisha kwa washindi wa washiriki wa mashindano hayo.

GM Lyambiko alisema mgodi huo utandelea kuwekeza katika michezo, ikiwa ni pamoja na kuanzisha timu za mashindano katika eneo hilo.

Alitumia fursa hiyo pia kuwashukuru na viongozi wote waliojitokeza kushiriki katika kilele cha mashindano hayo.

“Tunahamasisha mshikamano na upendo kwa faida ya pande zote mbili [wananchi na mgodi],” GM Lyambiko alisema.

Alibainisha kuwa bila mahusiano bora mgodi huo hauwezi kuendesha shughuli zake kwa utulivu na hata wananchi hawawezi kunufaika.

“Tunaamini kuwa bila mahusiano bora sisi kama mgodi hatuwezi kufanya kazi kwa utulivu na bila utulivu jamii haiwezi kunufaika,” alisema Lyambiko.

Kampuni ya Barrick imetumia pia mashindano hayo kukuza na kudumisha mahusiano mema kati ya mgodi huo na jamii inayouzunguka.

Mashindano hayo yatasaidia pia kuongeza uelewa juu ya fursa mbalimbali zilizopo na kushughulikia masuala mtambuka, hasa uvamizi, uharibifu wa miundombinu (vandalism) na utegeshaji wa mazao, miti na nyumba.

Chanzo: Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages