NEWS

Monday 19 September 2022

TPO Tarime yapeleka msaada kwa watu wenye uhitaji wanaotunzwa Mji wa Huruma Musoma


Na Mara Online News
------------------------------

TAASISI ya Kizalendo Tanzania (TPO) Wilaya ya Tarime imepeleka na kukabidhi msaada wa vitu mbalimbali kwa watu wenye uhitaji wanaotunzwa katika kituo cha Mji wa Huruma uliopo Kigera Etuma, Musoma Vijijini.

Wanachama wa TPO Wilaya ya Tarime wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Philipo Lusotola walikabidhi msaada huo mbele ya Msimamizi wa kituo hicho, Padre Biseko Pendo, Septemba 17, 2022.

Msaada huo umehusisha mchele kilo 200, sukari kilo 50, mbuzi wawili, unga wa ngano kilo 25, sabuni za miche boksi sita, sabuni za unga, mikungu ya ndizi, nguo zikiwemo koti na viatu.

Wanachama wa TPO Wilaya ya Tarime wakikabidhi msaada wa vitu mbalimbali. Kulia ni Msimamizi wa kituo cha Mji wa Huruma, Padre Biseko Pendo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Lusotola alisema wanachama wa TPO Wilaya ya Tarime wamechangishana fedha za kununua vitu hivyo kwa ajili ya watu wanaotunzwa kituoni hapo.

“Lakini pia, tunatoa msaada huu kuhamasisha watu wenye uwezo wa kiuchumi kujitokeza kusaidia ndugu zetu zaidi ya 100 wanaotunzwa katika kituo hiki cha Mji wa Huruma,” aliongeza.

Msimamizi wa kituo hicho, Padre Biseko aliwashukuru wanachama wa TPO Wilaya ya Tarime kutokana na msaada huo wa kibinadamu kwa ajili ya watu wanaotunzwa kituoni hapo.

Kwa mujibu wa Padre Biseko, kituo hicho kilianzishwa miaka 30 iliyopita na kinajiendesha kwa misaada kutoka kwa wahisani.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages