NEWS

Monday 10 October 2022

Mangalaya awashukuru wajumbe kumpa mitano tena Uenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Tarime



Na Mara Online News
---------------------------------

MWENYEKITI Mteule wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime, Samwel Mangalaya (pichani juu), amewashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya hiyo kwa kumrejesha madarakani kwa kipindi kingine cha miaka mitano ijayo.

“Ninawashukuru sana kunifanya nionekane mtu, bila ninyi mimi nisingekuwa kwenye kiti hiki, ninawashukuru sana, Mwenyezi Mungu awabariki, asanteni sana,” amesema Mangaraya katika kikao cha baraza la wazee wa jumuiya hiyo, kilichofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya CCM Wilaya ya Tarime, leo Oktoba 10, 2022.

Amesema kitendo cha wajumbe wa Mkutano Mkuu kumchagua tena kuwa Mwenyekiti kimedhihirisha imani yao kwake, hivyo naye atawatumikia katika misingi ya haki, kweli, utiifu na uaminifu mkubwa.

“Mimi ni mfia chama, ninaahidi nitakuwa mkweli kwenu, nitahakikisha uhai wa Jumuiya ya Wazazi unakuwepo na kujitolea kuhamasisha maendeleo yetu,” amesisitiza Mangaraya.


Katika kuonesha shauku yake ya maendeleo ya chama hicho tawala, Mangaraya ametangaza kwamba ametoa kiwanja chenye thamani ya shilingi milioni saba, kwa ajili ya kujenga ofisi ya Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime.

Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Tarime, ametumia nafasi hiyo pia kuwaomba wanajumuiya wenzake kuvunja makundi ya uchaguzi, kushirikiana kukijenga chama hicho na kutokubali kugawanywa.


“Ndugu zangu uchaguzi umeisha tukijenge chama, tuwe wamoja, makundi yote yarudi yajenge chama. Tumsaidie Rais Samia Suluhu Hassan, ni mchapa kazi, ni mama anayejitoa kwa ajili ya Watanzania, Mwenyezi Mungu ambariki na kumuongezea nguvu,” amesema Mangaraya.

Aidha, Mangaraya amewataka wanajumuiya hao kukaa mkao wa kula kwani anakusudia kuja na mpango mkakati wa kuhakikisha kila kata wilayani Tarime inaanzisha mradi wa kiuchumi kwa manufaa ya wanachama.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages