
Madeni ya umma barani Afrika yanaendelea kuwa changamoto kubwa kwa nchi nyingi, huku viongozi wa bara wakitafuta suluhu endelevu ya mgogoro huu unaokua kwa kasi.
Mwezi Mei 2024, Umoja wa Afrika uliandaa mkutano wake wa kwanza kuhusu madeni ya umma mjini Lomé, Togo, ambapo ilibainika kuwa zaidi ya nchi 20 za Afrika ziko katika hatari ya kuzidiwa na madeni.
Kwa mujibu wa Clever Gatete kutoka Tume ya uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (ECA), deni la nje la Afrika lilifikia takribani dola trilioni 1.86 mwaka 2024, ongezeko la zaidi ya dola bilioni 1,000 katika kipindi cha chini ya miaka kumi.
Kati ya mwaka 2015 na 2024, uwiano wa deni la Afrika kwa Pato la Taifa (GDP) ulipanda kutoka 44.4% hadi 66.7%, kwa mujibu wa Shirika la fedha dunian (IMF).
Takwimu za Oktoba 2025 zinaonyesha kuwa ongezeko hilo linaongozwa na: Sudan (272%), Senegal (128%) Zambia (115%) na Cape Verde (111%).
Wataalamu 25 huru walioteuliwa na urais wa Afrika Kusini chini ya mfumo wa G20 wamependekeza upunguzaji wa pamoja wa madeni na kuongeza uwekezaji ili kuimarisha maendeleo ya Afrika
Gatete anasisitiza kuwa: "Huu si tu mgogoro wa madeni, ni mgogoro wa maendeleo."
Kwa nchi nyingi, fedha ambazo zingetumika kwa maendeleo kwenye sekta za afya, elimu na miundombinu sasa zinaelekezwa kulipia madeni.
Nchi zenye madeni makubwa zaidi Afrika kwa uwiano wa deni/GDP
1. Sudan – 253% ya GDP
Sudan, ambayo inakabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, ina hali ngumu ya kiuchumi. Deni lake la umma au taifa limefikia 253% ya GDP, ambapo sehemu kubwa ni deni la nje kutoka kwa nchi za Ghuba na wanachama wa Paris Club.
2. Senegal – 119% ya GDP
Senegal ina deni la takribani dola bilioni 47.2, sawa na 119% ya GDP. Ripoti zinaonyesha kuwa deni la jumla likijumuisha mashirika ya umma linafikia 132% ya GDP, na hivyo kuiweka katika nafasi ya pili barani.
3. Zambia – 115% ya GDP
Mwisho wa 2024, deni la Zambia lilikuwa dola bilioni 21.4. Kwa mujibu wa IMF lilitarajiwa kupungua hadi 91.1% ya GDP mwaka 2025, lakini bado ni kati ya viwango vya juu zaidi barani.
4. Cape Verde – 109.4% ya GDP
Japokuwa deni lake limepungua kutoka 127.5% (2022), Cape Verde bado iko juu ya kiwango salama cha deni, na kufikia 109.4% ya GDP mwaka 2024.
5. Jamhuri ya Kongo – 93.6% ya GDP
Deni la Kongo limekuwa likipungua, lakini 93.6% ya GDP bado ni juu. Karibu nusu ya mapato ya serikali yalitumika kulipia madeni mwaka 2024.
6. Msumbiji – Zaidi ya 100% ya GDP
Mwisho wa 2024, deni lilifikia dola bilioni 16.238. Machi 2025, serikali ilitangaza kushindwa kulipa baadhi ya madeni, na IMF ikathibitisha kuwa deni limezidi 100% ya GDP.
7. Misri – 83% ya GDP
Misri ilitumia dola bilioni 21.3 kulipia madeni katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025, hali iliyoweka shinikizo kwa akiba ya fedha za kigeni.
8. Malawi – 88% ya GDP
Malawi ina deni la takribani dola bilioni 10.3, sawa na 88% ya GDP, na hivyo kuifanya kuwa miongoni mwa nchi zilizo na madeni makubwa katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika.
9. Mauritius – 88% ya GDP
Mauritius, ingawa ni miongoni mwa nchi zilizoendelea zaidi barani, ina kiwango cha juu cha deni – 88% ya GDP mwaka 2024.
Kiwango hiki kinabaki juu licha ya kupungua kutoka kilele cha 91.9% mwaka 2020.
10. Guinea-Bissau – 82.3% ya GDP
Guinea-Bissau, ambayo imekumbwa na misukosuko ya kisiasa, ina deni la taifa la 82.3% ya GDP mwaka 2024. Deni la ndani ni 55.5%, huku wakopeshaji wakubwa wa nje wakiwa ni Benki ya Dunia (30.2%).
Chanzo: BBC
No comments:
Post a Comment