NEWS

Tuesday 1 November 2022

Bodi ya Mikopo Elimu ya Juu isichezee WatanzaniaNa Mchambuzi Wetu
------------------------------

KATIKA hali ambayo haikutarajiwa, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) nchini, imeonywa vikali kutokana na kuinyima ushirikiano Kamati Maalum iliyoundwa na Serikali kuchunguza mwenendo wake katika utoaji wa mikopo kwa wanafunzi.

Onyo hilo lilitolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita.

Kamati Maalum iliyoundwa ilitangazwa na Waziri Mkenda Julai 31, 2022, ambapo ilielekezwa kufuatilia mwenendo wa HESLB katika utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, yaani kuanzia mwaka 2017/2018 hadi 2021/2022.

Ilianza kufanya uchunguzi huo Septemba 5, 2022 na ilitakiwa kuukamilisha ndani ya siku 30 zilizoishia mwanzoni mwa Oktoba 2022.

Kamati hiyo inaongozwa na Prof Allan Mushi ambaye ni Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro, huku wajumbe wake wakiwa ni Idd Makame kutoka Zanzibar na Dkt Martin Chegere, ambao wote ni wataalamu wa mifumo - waliobobea katika Sayansi ya Kompyuta na Takwimu.

Waziri Mkenda aliutangazia umma kwamba Serikali iliunda kamati hiyo kufanya uchunguzi huo ili kujua kama HESLB imekuwa ikitoa mikopo kwa haki, uwazi na kuzingatia vigezo stahiki.

Ikumbukwe kwamba Serikali ililazimika kuunda Kamati hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba HESLB imekuwa ikifanya upendeleo katika utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Kwamba Bodi hiyo imekuwa ikifanya upendeleo wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wasiokuwa na sifa zilizoainishwa kwenye utararibu mzuri uliowekwa na Serikali ili kunufaisha watoto wanaotoka familia zisizo na uwezo wa kugharimia masomo ya elimu ya juu.

Hivyo kitendo kinachoelezwa kuwa HESLB iliinyima Kamati hiyo ushirikiano ilipotembelea ofisi za Bodi hiyo maeneo ya Tazara jijini Dar es Salaam, ni cha hujuma na kinalenga kukwamisha juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha watoto wa Watanzania wanapata mikopo ya elimu ya juu bila upendeleo.

Ninasema kitendo hicho ni cha hujuma kwa sababu kinataka kuikwamisha Serikali katika dhamira yake ya kutaka malalamiko yaliyotolewa dhidi ya HESLB yapatiwe ufumbuzi.

Ni dhahiri kinachotaka kufanywa na Bodi hiyo ni kuichezea Serikali na Watanzania kwa ujumla katika kutafuta ufumbuzi wa malalamiko hayo kwa manufaa ya umma.

Kuna haja ya mamlaka za juu serikalini kuangalia uwezekano wa kuchukua hatua zaidi za kuibana HESLB itoe ushirikiano utakowezesha Kamati Maalum kukamilisha uchunguzi uliokusudiwa.

Pamoja na Waziri Mkenda kutoa onyo kali kiasi cha kutishia ‘kula kichwa cha mtu’ katika Bodi hiyo ya mikopo kama itaendelea kusuasua katika kutoa ushirikiano wa kuwezesha Kamati Maalum kufanya kazi yake, bado kuna haja ya Serikali kuona ulazima wa kutumia vyombo vyake maalumu kama vile dola kusimamia utekelezaji wa kazi hiyo.

Ikibidi viongozi na wafanyakazi wa HESLB waliohusika kukwamisha na kuchelewesha Kamati Maalumu ya Uchunguzi wahojiwe na vyombo vya dola na hata kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.

Ninasisitiza hili kwa sababu kama alivyosema Waziri Mkenda wakati akitoa onyo, huenda kuna ‘madudu’ ambayo Bodi hiyo inataka kuficha yasijulikane kwa Kamati ya Uchunguzi.

“Sisi tunataka kujisahihisha ili kuhakikisha kwamba kile ambacho Serikali imetenga kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi kinaenda kwa mlengwa, sasa ninataka kutoa onyo ya kwamba kwenda ku- lobby sijui eti Waziri asimamishe kamati isifanye kazi… hiyo lobbing inaonesha kuna madudu.

“Bungeni watu wanalalamika sana, wanasema kuna yatima hawapewi mikopo, halafu watu wenye uwezo wanapewa mikopo, mimi naunda kamati alafu nisikie kuna mtu anasema Waziri asiunde kamati, aah! Nitakula kichwa cha mtu,” alisisitiza Waziri Mkenda katika mkutano na waandishi wa habari.

Janjajanja inayotaka kuoneshwa na HESLB kipindi hiki cha uchunguzi maalum isipewe nafasi kwani Serikali inayoongozwa na Rais Samia imeongeza bajeti hadi kufikia shilingi bilioni 570 ili kuhakikisha kuwa vijana wa Kitanzania wanaokidhi vigezo hawakosi elimu ya juu kwa sababu ya wazazi wao kutokuwa na uwezo wa kuwasomesha.

Lazima kuwe na usimamizi, uangalizi, uwazi, haki na weledi wa hali ya juu katika utoaji wa mikopo ya elimu ya juu, ili walengwa waweze kunufaika nayo kama ilivyoelekezwa na Serikali, siyo vinginevyo.

Chanzo: Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages