Na Mara Online News
---------------------------------
MADIWANI wa Halmashauri ya Mji wa Tarime wameiomba ofisi ya Mkurugenzi kuangalia uwezekano wa kuwapatia wenyeviti wa mitaa katika halmashauri hiyo semina ya uongozi na utawala bora.
Wakitetea hoja hiyo kwenye kikao cha baraza lao - kilichofanyika Tarime Sekondari leo Novemba 2, 2022, madiwani hao wamesema wenyeviti wa mitaa wengi katika halmashauri hiyo hawajui majukumu yao ya uongozi.
Hoja hiyo imeibuliwa na Diwani wa Kata ya Sabasaba, Raymond Balenzo na kuungwa mkono na madiwani wote, wakisisitiza kuwa semina hiyo itawezesha wenyeviti hao kujua majukumu yao, ikiwa ni pamoja na kushirikiana na viongozi wengine kuhamasisha shughuli za maendeleo ya wananchi.
Wamelalamikia kasumba ya wenyeviti wa mitaa wengi kutoitisha mikutano ya wananchi ili kuhamasisha shughuli za maendeleo, hata pale wanapoelekezwa na maofisa watendaji wa meneo yao ya uongozi.
“Wenyeviti hawa hawajui majukumu yao, hivyo tunaomba wapewe semina ya uongozi na utawala bora wajue majukumu yao,” amesisitiza Diwani Balenzo.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Thobias Ghati amesema ikiwezekana kwanza, wenyeviti hao wakutanishwe na Mkurugenzi na Ofisa Utumishi wa Halmashauri hiyo kupewa maelekezo ya awali kuhusu majukumu yao.
Hata hivyo, Ghati ambaye ameongoza kikao hicho, amewataka madiwani kusaidia kuhimiza wenyeviti wa mitaa kuitisha mikutano ya wananchi ya kuhamasisha shughuli za maendeleo.
Makamu Mwenyekiti, Thobias Ghati akizungumza akikaoni. Aliyekaa ni Mkurugenzi Gimbana Ntavyo. (Picha zote na Mara Online News)
Badaye akizungumza katika kikao hicho kilichopokea na kujadili taarifa za kata za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Gimbana Ntavyo ameahidi kufanyia kazi hoja za madiwani hao.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi Ntavyo amewakumbusha watendaji wa halmashauri hiyo kuandaa taarifa kwa umakini ili kuepuka aibu ya kukosolewa na madiwani na kuomba msamaha vikaoni.
No comments:
Post a Comment