NEWS

Monday 28 November 2022

Kwanini Chandi anaweza kubadilisha Mara kuwa mkoa bora zaidi kwa uwekezaji nchini


Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa.

Na Mwandishi Maalumu, Musoma
-------------------------------------------------

LICHA ya kuwa na historia ya kutoa Rais wa Kwanza wa Tanzania, mkoa wa Mara umebarikiwa kuwa na maliasili muhimu nyingi ambazo zikitumika vizuri zinaweza kuubadili kuwa wenye maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii.

Mkoa wa Mara ndipo alipozaliwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na baadhi ya viongozi waliofanya naye kazi karibu.

Ni mkoa ambao kwa sehemu kubwa ni nyumbani kwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo imetangazwa kuwa Hifadhi Bora Barani Afrika kwa miaka minne mfululizo [2019, 2020, 2021 na 2022].

Mkoa huu umebarikiwa pia kuwa na utajiri mkubwa wa madini ukiwemo Mgodi wa Dhahabu wa North Mara mabao kwa sasa unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Lakini pia Mara ni miongozni mwa mikoa ya Kanda ya Ziwa yenye sehemu kubwa ya Ziwa Victoria na maeneo muhimu ya mazalia ya samaki.

Pia kuna ardhi yenye rutuba inayostawisha mazao mbalimbali - kama pamba, mahindi, mhogo, mkonge, ndizi na kahawa aina ya Arabica ambayo inatamba katika soko la dunia.

Kwa kifupi, Mara ni mkoa wenye fursa nyingi zikiwemo za kufanya biashara na nchi jirani ya Kenya kwa kuwa baadhi ya wilaya zake, hususan Tarime na Rorya zinapakana taifa hilo.

Habari njema ni kwamba hatimaye mkoa wa Mara umempata Mwenyekiti mpaya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Patrick Chandi Marwa.

Kada huyu wa CCM na mfanyabiashara maarufu kutoka wilaya ya Serengeti, aliibuka mshindi baada ya kuwabwaga washindani wake wawili katika uchaguzi uliofanyika mjini Musoma, wiki iliyopita.

Katika uchaguzi huo uliotamalaki amani, Chandi alivuna kura 635 na kuwashinda wagombea wenzake; Joshua Mirumbe aliyepata kura 433 na Leonard Kitwara (kura 11).

Mwenyekiti aliyepita, Samwel Kiboye “Namba Tatu”, jina lake ‘lilikatwa’ kwenye vikao vya juu vya chama hicho tawala - alipoomba kuteuliwa kutetea nafasi hiyo.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Chandi alisema yeye ni mpenda maendeleo na kwamba hiyo ndiyo itakuwa ajenda yake kubwa hata atakapopata nafasi ya kukutana na viongozi wa kitaifa, akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Alisema yeye hatakuwa kiongozi wa kuchongea watu kwa viongozi wa juu, bali atajikita katika kuhakikisha kuwa mkoa wa Mara unapiga hatua ya maendeleo ya kisekta kwa manufaa ya wana-Mara na taifa kwa ujumla.

“Mimi sitaenda kushtaki watu, ajenda yangu itakuwa ni maendeleo,” Chandi alisema na kushangiliwa na umati mkubwa wa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Mara.

Mwenyekiti huyo aliahidi kukitendea haki CCM na kuonesha ushirikiano mkubwa kwa wasisi wa chama hicho.

Aliahidi pia kusimamia maendeleo na demokrasia mkoani Mara na kuhakikisha CCM kinaendelea kuaminiwa na wananchi na kupata ushindi mnono katika uchaguzi mkuu ujao.

Aidha, Chandi aliahidi kushirikiana na viongozi wengine kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi katika mkoa huo wakiwemo watumishi wa Serikali.

Kilichofurahisha zaidi wana-CCM ni paamoja na kauli yake kwamba atashirikiana na wanachama aliochuana nao katika kuubadilisha mkoa huo kimaendeleo.

“Nawapongeza wote nilioshindana nao, nitawakaribisha nipate mawazo yenu mazuri ili kwa pamoja tujenge chama chetu na mkoa wetu wa Mara,” alisema Chandi.

Ahadi yake nyingine ni ya kuimarisha mahusiano ya chama hicho tawala na viongozi wa Serikali mkoani.

“Nitakuwa na ushirikiano mkubwa kati ya Chama na Serikali ili tujenge nyumba moja,” alisema Bosi huyo mpya wa CCM Mkoa wa Mara.

Wanachama wa CCM na wananchi wengi mkoani Mara wameeleza kuridhishwa na ushindi wa Chandi, wakimtaja kuwa ni mtu mwenye upendo, mwadilifu, msema kweli, mpenda haki na asiyebagua watu.

“Chandi ni mtu sahihi na mwenye upendo kwa kila mtu, hana ubaguzi wa kikabila. Moyo wake ni mweupe na ni msema kweli. Nadhani ataondoa makundi yaliyotengenezwa ndani ya CCM,” alisema mmoja wa wana-CCM.

Aliyekuwa mshindani wa karibu wa Chandi katika kinyang’anyiro hicho, Joshua Mirumbe aliahidi kushirikiana na Mwenyekiti huyo mpya katika kukijenga chama hicho mkoani Mara.

“Niko tayari kutoa ushirikiano wa kutosha ili CCM Mara iende vizuri zaidi,” alisema Mirumbe na kuongeza kuwa mkoa huo una changamoto nyingi zinazohitaji utatuzi wa haraka.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Christopher Mwita Gachuma ambaye alifanikiwa kutetea nafasi yake ya UNEC, alisema atakuwa mshauri mzuri wa Mwenyekiti Chandi ili kuleta mabadiliko makubwa ya kimaendeleo mkoani.

“Mimi sio mzee, mimi ni mtu mzima na akili zangu ziko sawa, hivyo ushauri wangu kwa Mwenyekiti utakuwa mzuri na wa haki,” alisema Gachuma ambaye pia ni mfanyabiashara maarufu Kanda ya Ziwa.

Chandi ana uzoefu wa uongozi na amewahi kushika nafasi mbalimbali ndani ya CCM.

Nafasi za uongozi ambazo Chandi amewahi kushika ndani ya CCM ni pamoja na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Mwenyekiti wa Wilaya ya Serengeti, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa, Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Mara na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama hicho Mkoa kupitia Vijana.

Chanzo: SAUTI YA MARA

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages