NEWS

Tuesday 29 November 2022

Wabunge wa Mara lawamani kwa kutohudhuria vikao vya maendeleo ya wananchi, RC Mzee, Katibu wa CCM wakerwaNa Mara Online News, Musoma
--------------------------------------------------

MAKATIBU wa wabunge wa mkoani Mara wametimuliwa na Mkuu wa Mkoa (RC), Meja Jenerali Suleiman Mzee (aliyesimama pichani juu) katika kikao cha Bodi ya Barabara cha mkoa huo, kwamba si wajumbe wa kikao hicho.

RC Mzee amewataka makatibu hao kuondoka katika kikao hicho leo Novemba 29, 2022 mjini Musoma, baada ya kubaini kuwa kati ya wabunge tisa wa majimbo na wawili wa viti maalum waliopo mkoani Mara, ni Mbunge wa Bunda Vijijini, Boniphace Getere pekee aliyehudhuria.

Kiongozi huyo ameonekana kukerwa na mazoea ya wabunge wengi wa mkoa wa Mara kutohudhuria vikao vya Bodi ya Barabara na vingine vinavyojadili maendeleo ya mkoa huo.

“Kikao hiki ni cha kisheria kiheshimiwe, wawakilishi wa wabunge waondoke siyo wajumbe wa kikao hiki. Mazoea haya yaachwe, sitakubali ubabaishaji huu katika mkoa huu.

“Ninawaomba wawakilishi wa wabunge waondoke au wakae kama wasikilizaji lakini sio kama wajumbe,” amesisitiza RC Mzee wakati akifungua kikao hicho, ambapo maelekezo yake hayo yametekelezwa kwa makatibu hao kuondoka kikaoni.

Hata hivyo, Bosi huyo wa mkoa ambaye ni Mwenyekiti wa kikao hicho ametoa wito wa kuwataka wabunge ambao hawakuhudhuria kikao hicho kuwasilisha kwake maelezo ya sababu za kutofika bila kutoa taarifa.


Baadhi ya wajumbe mbalimbali wa kikao hicho, akiwemo Katibu wa chama tawala - CCM Mkoa wa Mara, Lengael Akyoo waliunga mkono hatua hiyo ya RC Mzee wakitaka mazoea hayo ya wabunge yakomeshwe.

“Katibu wa mbunge hawezi kuleta mawazo tunayoyataka. Mbona bungeni hawawatumi makatibu kuwawakilisha,” amesema Akyoo.

Katibu huyo amesisitiza kuwa wabunge hawapaswi kutuma wawakilishi katika vikao vinavyojadili miradi mikubwa inayogharimu mabilioni ya fedha zinazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

“Haya tunayojadili hapa ndiyo yanayobeba ilani ya CCM. Ni heri kiti chake [mbunge] kikabaki wazi, na tukiruhusu hivi [akimaanisha wabunge kuwakilishwa vikaoni] tutakuwa tumeamua kukosa mawazo ya wabunge kwenye vikao hivi,” Akyoo amesisitiza.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dkt Vincent Mashinji amesema kitendo cha wabunge kutohudhuria kikao hicho kinaweza kuwa cha makusudi kwani wengi wao wapo majimboni wanaendelea na mambo yao. "Wengine wako mitaani, wengine tumepishana nao," amesema.

Wabunge ambao hawakuonekana kikaoni hadi wakati Mkuu wa Mkoa anachukua hatua hiyo ni Vedastus Mathayo wa Musoma Mjini, Profesa Sospeter Muhongo (Musoma Vijijini), Jumanne Sagini (Butiama), Robert Maboto (Bunda Mjini), Charles Kajege (Mwibara), Amsabi Mrimi (Serengeti), Mwita Waitara (Tarime Vijijini), Michael Kembaki (Tarime Mjini), Jafari Chege (Rorya), Ghati Chomete (Viti Maalum) na Agnes Marwa (Viti Maalum).

Mwenyekiti mpya wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa amehudhuria kwa mara ya kwanza kikao hicho.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages