Na Mara Online News
-----------------------------------
JESHI la Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime-Rorya limewatia mbaroni watuhumiwa 338 kwa mkosa mbalimbali yakiwemo ya kupatikana na dawa za kulevya, wizi wa mifugo, pikipiki, mawe ya dhahabu, uvamizi mgodini, huku likikamata pia bunduki mbili [shotgun, bastola] na risasi 82 za AK 47, kati ya Julai na Oktoba 2022.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Geofrey Sarakikya ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake leo Novemba 24, 2022.
“Mafanikio makubwa yamepatikana kutokana na misako na operesheni mbalimbali zilizofanyika katika wilaya zote sita [zinazounda mkoa huo wa kipolisi] ambazo ni Tarime, Sirari, Nyamwaga, Kinesi, Shirati na Rorya,” Kamanda Sarakikya amesema.
Kamanda Sarakikya (kushoto) akisoma taarifa kwa vyombo vya habari leo
Amechanganua kuwa kupitia misako na operesheni hizo jeshi hilo limeweza kukamata watuhumiwa 236 wakiwa na lita 2,370 za pombe haramu aina ya gongo, na wengine 35 wakiwa na bangi yenye uzito wa kilo 4,241 na pikipiki tisa zilizokuwa zinatumika kusafirisha bangi hiyo.
“Aidha, watuhumiwa watatu wamekamatwa kwa kumiliki mashamba ya bangi yenye ukubwa wa ekari 9.5 ambayo haadaye yaliteketezwa kwa moto, lakini pia watuhumiwa sita wamekamatwa wakiwa na mirungi yenye uzito wa kilo 80. Watuhumiwa hao wameshafikishwa mahakamani,” ameongeza.
Watu wengine 28 wamekamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya wizi wa mifugo na 20 kati yao tayari wameshafikishwa mahakamani na waliobaki watafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya upelelezi kukamilika, kwa mujibu wa ACP Sarakikya.
“Pia tumewakamata wahamiaji haramu tisa kwa makosa ya kuingia nchini bila kibali na tumewakabidhi katika Idara ya Uhamiaji kwa hatua za kisheria,” ameongeza kamanda huyo.
Aidha, Kamanda Sarakikya ametaja mafanikio ya jeshi hilo katika kesi zilizofunguliwa mahakamani kuwa ni pamoja na washtakiwa tisa wa unyang’anyi wa kutumia silaha kuhukumiwa kila mmoja kifungo cha miaka 30 gerezani.
Kuhusu kesi za ubakaji, amesema washtakiwa watatu wamehukumiwa kila mmoja kwenda jela miaka 30 na mmoja amehukumiwa kutumikia kifungo maisha gerezani.
Kwenye kesi za makosa ya kupatikana na nyara za Serikali, amesema washtakiwa watatu wamehukumiwa kila mmoja kutumikia kifungo cha miaka 20 jela.
“Pamoja na mafanikio yote hayo ya kuzuia, kupambana na kupunguza hofu ya uhalifu katika Mkoa wa Kipolisi Tarime-Rorya, Jeshi la Polisi mkoani hapa linaendelea kuishirikisha jamii kwa kutoa elimu kupitia vyombo vya habari, mikutano ya polisi jamii na mazoezi ya pamoja ya kila mwezi,” amehitimisha Kamanda Sarakikya.
No comments:
Post a Comment