NEWS

Wednesday 30 November 2022

Siasa: Nyota ya Joyce Mang’o yazidi kung’ara, achaguliwa UNEC Viti 3 Tanzania Bara


Joyce Ryoba Mang'o

Na Mara Online News
-------------------------------------

KADA kijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Joyce Ryoba Mang’o, ameng’ara kisiasa, baada ya kuibuka mshindi wa nafasi tatu za uongozi ndani ya chama hicho tawala.

Wiki iliyopita, Mang’o alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) Viti Vitatu Tanzania Bara kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).

Katika uchaguzi huo, mwanachama maarufu, Mary Chatanda alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa UWT Taifa, akimshinda kwa mbali Gaudentia Kabaka aliyekuwa anatetea nafasi hiyo.

Chatanda ambaye amewahi kuwa mbunge, anatajwa kuwa ni mmoja wa wanasiasa wanawake wenye mvuto na wachapakazi.

Kwa upande mwingine, Mang'o katika chaguzi nyingine alifanikiwa kushinda nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa UWT Taifa na Mjumbe wa Baraza la UWT Mkoa wa Mara kutokea wilaya ya Tarime.

Itakumbukwa kwamba Mang’o alikuwa mmoja wa watia nia ya Ubunge Jimbo la Tarime Vijijini kwa tiketi CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

Hata hivyo, pamoja na kura za maoni kutotosha, Mang'o alirudi kusaidia kampeni za chama na akawa Meneja Kampeni za Ubunge Jimbo la Tarime Mjini zilizomwezesha Michael Kembaki (CCM) kuibuka mshindi wa nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Desemba 28, 2020.

Lakini pia Mang'o ameendelea kushirikiana na viongozi na wanachama wa CCM wilaya ya Tarime na mkoa wa Mara katika kuhamasisha na kukuza uhai wa chama hicho tawala.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages