NEWS

Tuesday 29 November 2022

CCM Taifa yalaani kitendo cha mwanachama wake kudhalilishwa na kada wa CHADEMA Tarime



Na Mara Online News
----------------------------------

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Taifa kimelaani vikali kitendo cha mwanachama wake kudhalilishwa na kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Tarime, Mara.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na CCM Taifa jana, ilisema kitendo hicho ni ukiukwaji mkubwa wa utu, haki za binadamu na uhuru wa Mtanzania kuamini katika itikadi ya chama cha siasa anachokitaka.

“Chama Cha Mapinduzi kimesikitishwa na kinalaani vikali sana kitendo cha udhalilishaji na utwezaji wa haki ya msingi ya Mtanzania kuamini katika imani ya chama chake cha siasa bila kuingiliwa kama kilivyofanywa na kuonekana katika ‘video clip’… kilichomhusisha mwanachama wa CHADEMA, Mwalimu Chacha Heche.


Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mwalimu Chacha Heche ni kaka wa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA [aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini].

“Video hiyo inamuonesha Bwana Chacha akimlazimisha mzee mmoja kuvua fulana yenye nembo ya Chama Cha Mapinduzi aliyoivaa kwa mapenzi yake binafsi. Kijana huyo ameonekana akimtweza na kumlazimisha kuvua fulana hiyo ya CCM ili kuweza kumpa ajira mzee huyo na asipofanya hivyo basi angemfukuza.

“Mtanzania yeyote ana haki ya kuvaa nguo ya chama chochote cha siasa akipendacho bila kunyanyaswa au kubaghuliwa na yeyote yule,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa - Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka (pichani juu).

Kulingana na taarifa hiyo, kitendo kilichofanywa na Mwalimu Heche pia kinakwaza juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha Watanzania wanakuwa wamoja bila kubaguana kwa misingi ya itikadi za kisiasa.

“Tuna imani mamlaka husika zitachukua hatua kali za kisheria kwa unyanyapaa wowote dhidi ya Mtanzania yeyote atakayefanyiwa vitendo vyovyote vya unyanyasaji katika nchi yake, kama alivyofanyiwa mzee huyu anayeonekana katika video ile,” ilihitimisha taarifa hiyo ya CCM Taifa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages