NEWS

Tuesday 13 December 2022

Barrick yakanusha madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu North Mara

 Na Mwandishi Wetu

Kampuni ya Barrick imekanusha madai ya Kampuni ya  kisheria ya Leigh Day ikishirikiana na shirika la RAID la Uingereza kuhusu vifo vya watu wawili vinavyodaiwa kutokea katika Mgodi wa North Mara hivi karibuni.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo na Rais ambaye pia ni CEO wa  Barrick, Mark Bristow(pichani juu), imesema Kampuni yake inajivunia  rekodi nzuri ya Haki za Binadamu duniani kote na uhusiano mzuri kazini katika mgodi wake wa North Mara, pamoja na jamii zote zinazouzunguka.

Rais na CEO huyo ameongeza kwamba wafanyakazi wengi mgodini wanatoka katika vijiji jirani na hii ni sera ya kampuni hiyo na kwamba wengi wa wana vijiji hutii sheria japo kuna wachache wanaokwenda kinyume na hayo. 

‘’ Mwezi uliopita, wavamizi wapatao 100 wakiwa na mapanga  walijaribu kuruka ukuta wa North Mara  wenye urefu wa mita tisa ili kuiba mchanga wenye dhahabu na kuharibu miundo mbinu.  Kiasi cha wavamizi 71 walifanikiwa kuingia mgodini. 

Kwa vile walinzi wa mgodini hawana silaha, ilibidi kuomba msaada wa polisi ambao walipambana na wavamizi, kwa bahati mbaya mvamizi mmoja alifariki,’’ alisema Bristow.

Taarifa hiyo iliongeza kwamba madai ya RAID hayana msingi kwa sababu jeshi la Polisi Tanzania linaendeshwa kwa mujibu wa sheria zake na wala sio kwa kuongozwa au kutumwa na Kampuni ya Barrick.

Akionyeshwa kusikitishwa na mwenendo wa RAID, Rais huyo na CEO wa Barrick amesema shirika hilo lina historia ndefu ya kutoa madai yasiyokuwa na msingi kuhusu kile kinachodaiwa kuwa ukiukwaji wa Haki za Binadamu katika mgodi wa North Mara.

Bristow ameongeza kwamba hii inaweza kusababisha wananchi wasioelewa kupata fursa ya kuvunja sheria na hatimaye kuleta madai ya fidia.

Amesema kwa vile RAID haina makazi nchini Tanzania,amejaribu sana kuwakaribisha waje  mgodini wajionee wenyewe,lakini hawajawa tayari kufanya hivyo.

‘’Mwezi uliopita, kikao kilichokuwa kimepangwa kati ya Barrick na RAID kiliahirishwa masaa 48, kabla ya kufanyika. Hata hivyo bado tuko tayari  kuwakaribisha waje kuongea madai yao mbele ya polisi na hata wenyeji.

‘’Napenda kusema kwamba tumefanya kikao na viongozi 11 wa vijiji vinavyozunguka mgodi na wamekiri kutoifahamu RAID na kuongeza kwamba madai yao hayana msingi,’’ alisema Bristow.

Taarifa hiyo imehitimisha  kwa kusema kuwa wengi wa wafanyakazi wa mgodi wa North Mara wanatoka kwenye vijiji vilivyo jirani na mgodi huo na kusisitiza kuwa mgodi huo una mahusiano mazuri na jamii ambayo yanazidi kuimarishwa kupitia uwekezaji wa miradi ya kijamii  katika sekta za afya , elimu na miradi ya maendeleo ya miundo mbinu.



No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages