Na Mara Online News
------------------------------------
MKUU wa Wilaya (DC), Kanali Michael Mntenjele, Katibu Tawala wake, John Marwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Gimbana Ntavyo (pichani juu) wameungana na watumishi wengine wa Serikali kufanya usafi wa mazingira.
Viongozi hao wameshiriki shughuli hizo katika maeneo ya soko la ndizi la Rebu mjini humo mapema leo Desemba 8, 2022, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania yatakayofanyika kesho Desemba 9, 2022.
“Tumeamua kufanya usafi katika eneo hili la soko la Rebu leo kama sehemu ya kuadhimisha Siku ya Uhuru. Jana tulianza kwa kupanda miti kwenye eneo la hifadhi ya mto Mara,” amesema DC Mntenjele.
Naye Mkurungezi Gimbana amesema wamefanya hivyo pia kutekeleza utaratibu ambao Halmashauri ya Mji wa Tarime imejiwekea - wa kufanya usafi wa mazingira kila mwisho wa mwezi.
“Tumekuwa tukiwatangazia wananchi wa mji wa Tarime kuhakikisha usafi unafanyika. Leo tumependekeza eneo hili [soko la Rebu] ili wafanyabiashara wa hapa waone mfano na hivyo waendelee kuweka mazingira haya katika hali ya usafi,” amesema Gimbana.
No comments:
Post a Comment