NEWS

Friday 9 December 2022

Maadhimisho ya Miaka 61 ya Uhuru: Mbunge Chege awakutanisha watumishi Rorya kwenye bonanza la michezo na mdahalo


Na Mara Online News, Shirati
----------------------------------------------

KATIKA kuadhimisha Miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania leo Desemba 9, 2022, Mbunge wa Rorya mkoani Mara, Jafari Chege ameandaa na kudhamini bonanza la michezo mbalimbali baina ya watumishi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya (Serikali Kuu) na Halmashauri ya Wilaya (Serikli za Mitaa).

Mashindano ya michezo hiyo ikiwemo mpira wa miguu, kuvuta kamba, kuendesha baiskeli na kufukuza kuku, yamefanyika leo kwenye viwanja vya Obwere - Shirati wilayani Rorya.

Lengo la mashindano hayo, kwa mujibu wa Mbunge Chege, ni kuboresha mahusiano baina ya watumishi hao na wananchi kwa ujumla.

Ameongeza kuwa mahusiano mazuri, usirikiano na bidii ya kazi ni silaha muhimu ya kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika halmashauri hiyo inayopakana na Ziwa Victoria.

“Ningependa kusaidia kudumisha mahusiano ya watumishi wetu ili wapate molari ya kufanya kazi kwa upendo na kujituma,” amesema Chege katika mazungumzo na Mara Online News.

Mbunge wa Rorya, Jafari Chege.

Mbali na mashindano mengine, kumekuwepo na mechi maalumu kati ya mashabiki wa Yanga na Simba.

Baadaye kumekuwepo na mdahalo maalumu wa viongozi na wananchi wa kada mbalimbali uliofana kwa aina yake katika ukumbi wa Hoteli ya 2000 Shirati.

Mdahalo huo umejikita katika kuzungumzia amani na umoja kama nguzo ya maendeleo ya Watanzania, ambapo viongozi wa kimila, dini na watoa mada mbalimbali wameelezea jinsi Taifa la Tanzania lilivyopiga hatua za kimaendeleo katika miaka 61 ya uhuru, lakini pia maendeleo ya Rorya kwa miaka 15 baada ya kujitenga kutoka wilaya ya Tarime.

Washiriki waliozungumza na Mara Online News wamempongeza Mbunge Chege wakisema hatua hiyo ya kuwakutanisha watu wa kada tofauti katika bonanza la michezo, mdahalo na chakula cha pamoja imewawezesha kufahamiana na kujenga uhusiano.

“Haya ni miongoni mwa maono makubwa ya Mheshimiwa Mbunge wetu ambayo ameendelea kuyadhihirisha katika wilaya yetu ya Rorya, hasa ukizingatia tangu ameingia madarakani amekuwa akifanya vitu vingi ambavyo wananchi wanaviona na kukubaliana navyo,” amesema Mwalimu Mjinja John Magambo kutoka Shule ya Msingi Rayori.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages