Na Mara Online News, Nyamongo
---------------------------------------------------
MAELFU ya wanafamilia wa wafanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kutoka mikoa mbalimbali nchini Tanzania, wameungana kuadhimisha Siku ya Familia (Family Day) mgodini hapo leo Desemba 17, 2022.
Maadhimisho hayo yamepambwa na maonesho ya shughuli zinazofanyika katika mgodi huo, michezo mbalimbali ya watu wakubwa na watoto, chakula cha pamoja, vinywaji na muziki.
Mgodi wa North Mara upo eneo la Nyamongo katika wilaya ya Tarime mkoani Mara, ukiendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
Mwenyeji wa maadhimisho hayo ya Siku ya Familia, Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko ameongoza msafara wa mgeni rasmi, akiwemo Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara kutembelea mabanda ya maonesho ya shughuli za mgodi.
Mbunge Waitara (wa pili kushoto) akisikiliza maelezo kuhusu kifaa cha uokozi kutoka kwa mfanyakazi wa mgodi wa North Mara. Wa kwanza kulia ni GM Lyambiko.
Hotuba ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele imeeleza kufurahishwa na namna mgodi huo unavyojali familia za wafanyakazi wake kiasi cha kuwaalika kwenda kuona wanavyofanya kazi.
“Nimeelezwa kwamba mkusanyiko huu unajumuisha wanafamilia zaidi ya 2,000 kutoka kila kona ya Tanzania. Ni jambo la faraja sana kutembelewa na familia,” imesema sehemu ya hotuba ya Kanali Mntenjele na kuipongeza Kampuni ya Barrick kwa kujijengea utaratibu huo.
“Tumeendelea kuwa na ushirikiano mzuri na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara. Kwa niaba ya Serikali niwaahidi kuendelea kushirikiana nanyi katika kuhakikisha mnafikia dhamira yenu katika viwango vya juu zaidi,” imeongeza sehemu ya hotuba ya Kanali Mntenjele.
Ikaongeza kuwa ni matumaini yake kwamba Barrick North Mara itaweza kufikia malengo yake kwa kuendelea kuyapa kipaumbele maadili ya msingi ya kuwa na usalama mahala pa kazi wakati wote,
“Uwajibikaji na uadilifu, matokeo chanya, ubia, kuwa na watu wa kiwango cha kimataifa, ukweli, uwazi na uadilifu yatafanya mfikie dhamira yenu,” imesema sehemu ya hotuba ya Mkuu huyo wa Wilaya.
Ikaongeza kuwa kaulimbiu ya Siku ya Familia ya Barrick North Mara 2022 inayosema “Kazi na Familia” inaakisi dhamira ya Serikali ya kutaka watu wafanye kazi kwa kujituma huku wakikumbuka malezi bora kwa familia zao.
“Nimefarijika kuwaona hapa viongozi wa vijiji vinavyozunguka eneo la mgodi. Sisi kama Serikali kupitia mkusanyiko huu tunahamasisha mshikamano, ujirani mwema, amani na upendo kati ya mgodi na vijiji vinavyouzunguka.
“Mshikamano huu utazidi kujenga urafiki na hivyo kuleta faida kwa pande zote, yaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwekezaji wetu Barrick na wananchi wanaozunguka mgodi,” ameongeza sehemu ya hotuba ya Kanali Mntenjele.
No comments:
Post a Comment