NEWS

Sunday 4 December 2022

Mkuu wa Hifadhi ya Serengeti asema askari hawakulenga kuua ng’ombe, walilazimika kufyatua risasi kuokoa maisha yao



Na Mara Online News
------------------------------------

MKUU wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Izumbe Msindai (pichani juu), amesema askari wa hifadhi hiyo walilazimika kufyatua risasi ili kujihami na hawakulenga kuua ng’ombe walioonekana kwenye mitandao ya kijamii wakiwa wamekufa.

Kwa mujibu wa Mhifadhi Msindai, tukio hilo lilitokea Desemba 2, 2022 baada ya askari hao kukamata mifugo ndani ya hifadhi katika eneo lenye mgogoro kati ya hifadhi na vijiji vya Kegonga na Nyandage wilayani Tarime, Mara.

Amesema baada ya askari kukamata mifugo ndani ya hifadhi walikumbana na mashambulizi kutoka kwa watu waliokuwa wanataka mifugo iachiwe, ndipo wakajihami kwa kurusha sisasi.

“Askari hawakuwa na lengo la kuua mifugo, walilazimika kurusha risasi kuokoa maisha yao na mali za Serikali pia,” amedai Msindai katika mazungumzo na Sauti ya Mara kwa njia ya simu jana Jumapili jioni.

Ameongeza kuwa mashambulizi yaliyotokea wakati wa tukio hilo yalikuwa makali, hayakuwa ya kawaida.

Kulingana na Mhifadhi huyo, baada ya tukio hilo askari hao ambao amesema walikuwa wanatekeleza majukumu yao kisheria, waliondoka eneo hilo na kwamba hadi wanaondoka hawakuona ng’ombe walioanguka na kufa.

Aidha, amesema wanaendelea kuimarisha ulinzi kwenye maeneo yote ya mpaka wa hifadhi hiyo.

“Nawashauri wananchi watambue na kuheshimu maeneo yaliyotengwa kisheria kama hifadhi na wayatumie maeneo hayo kujiendeleza kiuchumi badala ya kumnufaisha mwananchi mmoja mmoja,” amesema.

Mhifadhi Msindai amesema eneo hilo ni zuri kwa uwekezaji wa kitaalii ambao unaweza kuwanufaisha wakazi wa vijiji hivyo na kuharakisha maendeleo yao ya kiuchumi na kijamii.

Wakati huo huo, amesema hivi karibuni Shirika la TANAPA kupitia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti lilitoa shilingi zaidi ya milioni 70 kugharimia ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na nyumba ya mwalimu katika Shule ya Msingi Kegonga kupitia mpango wake wa ujirani mwema.

“Kama hifadhi tunaendelea kutoa elimu na kushirikisha wananchi wa vijiji vilivyo jirani ili waweze kunufaika na uwepo wa hifadhi hii,” ameongeza Mhifadhi Msindai.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara akihutubia mikutano ya hadhara kijijini Masanga wiki hii, amewasihi kuacha kupeleka mifugo kuchunga ndani ya hifadhi kwani kufny hivyo ni kuvunja sheria.

Mbunge huyo amewambia wanavijiji kuwa sheria inazuia mifugo kuingia ndani ya hifadhi na ndio maana kila ng’ombe anapokamatwa hifadhini mmiliki husika hutozwa faini shilingi laki moja, au mifugo yake kutaifishwa na Serikali.

“Mimi sitaki watu wangu wafilisike, ukitaka kumsaidia mtu mwambie ukweli,” Waitara amesisitaza na kuwataka wananchi hao kupuuza maneno ya aliowaita wanasiasa wahuni, ambao hawawambii ukweli kuwa kuchunga ndani ya hifadhi ni kuvunja sheria.

Ameweka wazi kuwa kuanzia sasa hatahusika kusaidia ufuatiliaji wa mifugo itakayokamatwa ikichunga ndani ya hifadhi hiyo, huku akiwatupia lawama wananchi ambao wamekuwa wakikaidi katazo la kutopeleka ng’ombe hifadhini.

“Kuanzia leo mkichunga kwenye hifadhi, mimi sitaonekana, haitatokea, haiwezekani kila siku ni kesi. Mimi habari ya kesi sitafanya, mimi nitatetea wanaoonewa. Hifadhi, watu na mifugo yao vyote ni muhimu,” amesisitiza kiongozi huyo wa wananchi.

Amesema hakuna mbunge mwenye nia njema anayeweza kusimama na kuwaelekeza wananchi kuchunga ndani ya Hifadhi ya Taifa kama Serengeti, akisema wanaweza kufanya uchochezi huo ni matapeli wa kisiasa.

“Inabidi tuishi kwa akili sana, mkidanganywa mtakuwa masikini. Mimi siwezi kuwadanganya kwamba mwende kuchunga hifadhini. Faini ya kila ng’ombe ni shilingi laki moja, au faini na mwenye mifugo kufungwa na mifugo yake kutaifishwa,” Waitara amewambia wananchi hao.

Kuhusu mpaka kati ya wanavijiji hao na Hifadhi ya Serengeti, Mbunge Waitara alisema suala hilo ameshalifikisha kwa viongozi wa juu serikalini na litapatiwa ufumbuzi.

“Hili suala lipo serikalini, tusubiri tutapitia mpaka vizuri, sheria itekelezwe na majadiliano yawepo. Nimepeleka maombi yangu ili tupate namna ya kuishi salama na hifadhi iendelee kuwepo.

“Kwa hiyo ndugu zangu nataka niwashauri vizuri kwamba jambo hili ni la kisheria, nimeshapeleka hoja serikalini. Nimeomba mawaziri waje hapa wafanye mkutano na wananchi tupate ufumbuzi, hivyo msivamie hifadhi, huo ndio msimamo wangu” amehitimisha Mbunge Waitara.

Walipoulizwa na mbunge wao huyo kama wamemuelewa na kukubali maelekezo yake ya kuwataka kuacha kupeleka mifungo kuchunga ndani ya hifadhi hiyo, wananchi waliohudhuria mkutano huo walikubali kwa pamoja.

Mbunge Waitara akihutubia mkutano wa hadhara kijijini Masanga

Akihutubia mkutano mwingine wa hadhara kijijini Itiryo siku moja baadaye, Mbunge huyo wa Tarime Vijijini aliwataka wanavijiji kuheshimu maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya njia ya mifugo.

“Watu wameambiwa hii ni sehemu ya kupitisha mifugo, lakini wengine wamekwenda wamepanda katani na wengine wamejenga makazi hapo hapo,” Waitara amesema kwa mshangao na kuongeza:

“Lazima tuambizane maneno magumu, ukivunja sheria, sheria ichukue mkondo wake.”

Inaelezwa kuwa wanavijiji wamekuwa wakiingiza mifugo hifadhini na hivyo kusababisha migogoro kati yao na wahifadhi. Aidha, mifugo imekuwa ikikamatwa, kupigwa faini na kutaifishwa, na hivyo kuongeza umaskini kwa wananchi hao.

Baadhi ya vijiji vya wilayani Tarime vilivyopo jirani na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni Masanga, Kegonga, Nyandage, Karakatonga, Kenyamsabi na Gibaso.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages