NEWS

Thursday, 22 December 2022

RUWASA Tarime kutekeleza miradi mitano mipya ya maji


Na Mara Online News
-----------------------------------

WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Tarime mkoani Mara itatekeleza miradi mitano mipya ya maji kwa gharama ya shilingi bilioni 4.545 zilizotolewa na Serikali kwa mwaka wa fedha 2022 na 2023.

Hayo yameelezwa na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tarime, Mhandisi Malando Masheku (pichani) katika kikao cha kutoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa huduma ya maji ya bomba kilichowashirikisha wadau mbalimbali mjini Tarime, hivi karibuni.

Mhandisi Masheku ametaja maeneo ambayo miradi hiyo mipya itatekelezwa kuwa ni Nyamwaga, Kemakorere, Regicheri, Tagota na Ilinuno-Mnagusi.

Amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza mtandano wa miradi ya maji iliyo chini ya RUWASA Tarime kwa asilimia 16 na kwamba upatikanaji wa huduma ya maji ya bomba katika wilayani kwa sasa ni asilimia 73.3.

Meneja Masheku ametumia nafasi hiyo pia kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuendelea kuipatia wilaya ya Tarime fedha za kugharimia utekelezaji wa miradi na uboreshaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele aliyewakilishwa na Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wa Wilaya hiyo, Tito Masele, ameipongeza RUWASA kwa juhudi inazofanya kuboreshea wananchi huduma ya maji.

Aidha, ameitaka RUWASA kutumia wataalamu wa ndani na kuwapa kipaumbele wananchi wenyeji katika nafasi za vibarua wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo mipya na kwa kuzingatia jinsia ili kuwaongezea kipato.

Ametumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa miradi hiyo, lakini pia kutunza vyanzo vya maji na kulinda miundombinu yake kwa manufaa yao.

“Serikali inatumia fedha nyingi kuhakikisha wananchi wanapata hudum bora ya maji, hivyo hatutasita kuchukua hatua kali kwa watakaokwamisha na kuharibu miradi ya maji na miundombinu yake,” amesisitiza Kanali Mntenjele katika hotuba yake.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages