NEWS

Monday 26 December 2022

TANROADS inavyong’arisha na kupendezesha miji, vijiji mkoani MaraNa Christopher Gamaina, Mara
------------------------------------------------

WANANCHI wa mkoani Mara wameeleza kufurahishwa na uwekaji wa taa za barabarani katika senta za miji na vijiji - unaotekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Wakiwemo wafanyabiashara mbalimbali, wanaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, wakisema uwekaji wa taa hizo umekuwa na faida nyingi kwao.

Wanasema katika mazungumzo na Sauti ya Mara wiki iliyopita kwamba taa hizo zimeuongezea hadhi na kuufanya mkoa wa Mara kuendelea kuwa sehemu bora ya watu kuishi na kufanya biashara.

“Tunaishukuru sana Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutuwekea taa za barabarani,” anasema Elizabeth Mathayo, mmoja wa wafanyabiashara wakubwa katika Manispaa ya Musoma.

Anaendelea “Taa hizi zimekuwa msaada mkubwa hata kwa wafanyabiashara wadogo kwani sasa wanafanya kazi hadi usiku bila woga maana kunakuwa na mwanga wa kutosha.”

Elizabeth ambaye ni mke wa Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Vedastus Mathayo, anaongeza kuwa taa hizo zimesaidia pia kuimarisha ulinzi na uslama nyakati za usiku.

“Taa za barabarani zimesaidia kupunguza vibaka, wananchi wanatembea usiku na kufanya shughuli zao kwa amani,” anasema Elizabeth.


Kwingineko katika senta ya kijiji cha Nyanchabakenye wilayani Rorya, wananchi wanaipongeza TANRODS na Serikali wakisema taa hizo zimeongeza usalama kwa wanakijiji wakiwemo wanaowahi usafiri alfajiri na wanaorudi usiku.

“Kwa ujumla hizi taa zimekuwa mkombozi katika kijiji chetu, maana pia zimechochea ukuaji wa uchumi, ambapo sasa hivi wananchi wanafanya biashara hadi usiku - tofauti na siku za nyuma.

“Wananchi wa Nyanchabakenye tuna kila sababu ya kuishukuru Serikali yetu chini Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jambo hili, bila kuisahau TANROADS kwa kazi nzuri,” anasema mkazi wa Nyanchabakenye, Siproza Charles Nyadhi.

Wanachama na viongozi wa chama tawala - CCM nao wanaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa fedha za kugharimia uwekaji wa taa za barabarani katika senta za miji na vijiji mkoani Mara, wakisema ni hatua nzuri ya maendeleo.

“Tunaishukuru sana Serikali yetu maana ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya CCM,” anasema Marema Sollo, mkazi wa senta ya Rebu katika mji wa Tarime.

Sollo ambaye pia ni Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Tarime, anasema ujio wa taa hizo siyo tu umesaidia kupendezesha mji huo - bali umeongeza fursa kwa wafanyabiashara kuendesha shughuli zao hadi usiku.

Wananchi wanaoishi na kufanya biashara katika senta zilizowekewa taa hizo wanasema zimesaidia pia kukomesha matukio ya vibaka kupora watu mali mbalimbali - yaliyokuwa yakichangiwa na giza nyakati za usiku.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe, anabainisha kuwa taa hizo zinawekwa kwenye senta zote za miji na vijiji katika barabara kuu na za mkoa.

“Tunaweka taa hizi kwenye senta zote za miji na vijiji kwa lengo kuu la kusaidia kuimarisha ulinzi, usalama na kuchochea shughuli za kibiashara, lakini pia kupendezesha maeneo hayo,” anasema Mhandisi Maribe katika mazungumzo na Sauti ya Mara ofisini kwake, wiki iliyopita.

Mhandisi Vedastus Maribe

Anasema taa hizo zinatumia umeme jua (solar) na kwamba zina uwezo wa kujiwasha kuanzia saa moja jioni hadi asubuhi kila siku.

Mhandisi Maribe anatumia nafasi hiyo pia kutoa wito wa kuwaomba wananchi kulinda usalama wa taa hizo katika maeneo yao kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

“Ombi letu kubwa kwa wananchi ni kwamba watunze hizi taa za barabarani kwa manufaa yao,” anasisitiza Meneja huyo wa TANROADS Mkoa wa Mara.

Adha, anaonya kuwa mtu yeyote atakayebainika kuharibu taa hizo kwa namna yoyote ile, ikiwemo kuzigonga na kuziiba atachukuliwa hatua kali za kisheria.


Mhandisi Maribe anataja wilaya ambazo tayari zimenufaika na mpango huo kuwa ni Bunda, Musoma, Rorya na Tarime.

Hatua hiyo inachochea maendeleo ya kiuchumi katika mkoa wa Mara uliobarikiwa kuwa na maliasili nyingi zikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, madini, Ziwa Victoria na ardhi yenye rutuba inayostwisha mazao mbalimbali kama kahawa aina ya Arabica inayotamba katika soko la dunia.

Kwa mujibu wa Mhandisi Maribe, TANROADS Mkoa wa Mara inahudumia mtandao wa barabara kuu zenye urefu wa kilomita 409.73, kati ya hizo, kilomita 194 ni za kiwango cha lami na kilomita 215.73 ni za changarawe.

Chanzo: Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages